Tanzania yaihitaji muda kunufaika na Mtangamano wa EAC-Makinda

Spika wa Tanzania, Anne Makinda

Na James Gashumba, EANA-Kigali

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda amesema Tanzania inahitaji muda zaidi wa kujipanga ili kujikita kikamilifu katika mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Alisema Tanzania ni nchi kubwa yenye mipaka mipana na watu zaidi ya milioni 45 hivyo kuingia katika mtangamano kikamilifu bado ni mapema mno na kunahitajika muda zaidi,linaripoti Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA).

‘’Siyo kwamba tunasita kufanya hivyo.Isipokuwa bado hatujawa tayari na tunahitaji muda zaidi.Kuna haja kwanza ya kuzungumza na watu wetu na kuwaelimisha kwa makini ili tunapoingia kusiwe na wasiwasi wowote,’’ Makinda alisema Jumatatu katika Mkutano wa Maspika wa Mabunge ya Kitaifa wa nchi za EAC uliofanyika Kigali, Rwanda Jumatatu.

Alifafanua kwamba suala la mtangamano ni zuri lakini pia ni muhimu kuanza katika msingi imara hususan ni kwa Tanzania. Makinda ilieleza kwamba nchi yake ina changamoto ya kuwaelimisha kwanza wananchi wake waelewe ili kuwa na mtangamano endelevu.

Tanzania, alisema inataka kwanza ihakikishe kwamba wananchi wake wanapata vitambulisho vya taifa kabla ya kujitumbukiza katika sera nyingine zaidi za mtangamano.Alidokeza kwamba inaweza ikachukua miaka miwili kupatikana kwa vitambulisho vya taifa.

Hata hivyo, Rais wa Baraza la Seneti la Rwanda, Dk. Jean Damascene Ntawukuriryayo alisema wabunge hawana budi kujitahidi kwa kadiri wawezevyo kuharakisha mchakato wa mtangamano.

Alisema pamoja na ukweli kwamba uvumilivu unahitajika pia ni muhimu kuhakikisha kwamba mambo yaliyopangwa yanatimizwa kwa wakati kama nchi wanachama wataka kunufaika na mtangamano.

“Tuhitaji kufikia malengo tuliyokubaliana na kama hatutaharakisha mchakato huo, tutapoteza mwelekeo na wengine wanaweza kujiuliza kwa nini tulianza mchakato huo,’’alisisitiza.

Spika wa Bunge la Kenya, Kenneth Marende amepongeza maendeleo yaliyokwisha fikiwa juu ya mtangamano mpaka sasa na kusema yanaridhisha na kwamba hakuna sababu ya kuwa na hofu na kusisitiza kuwa suala la kuwa tofauti miongoni mwa nchi wanachama halina nafasi katika siku za usoni.

Naye Spika wa Bunge la Uganda, Rebeka Kadaga alisema nchi wananchama wana ratiba tofauti za kuendesha masuala ya kisiasa na kwamba ipo haja ya kuoanisha shughuli hizo.

Akichangia hoja hiyo Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) anayemaliza muda wake, Abdirahin Abdi alisema kuilaumu nchi moja kwamba inachelewesha mchakato wa mtangamao si sawa na kuongeza kwamba hakuna hata nchi moja mwanachama iliyotekeleza kikamilifu itifaki ya Soko la Pamoja ikiwa ni pamoja na kuoanisha pia baadhi ya sheria.

“Ni kweli hatuendi kwa kasi ile ambayo tunataka lakini hatuna budi kuchambua masuala yanayouzunguka mtangamano huo kabla ya kuanza kulaumu nchi mwanachama binafsi,’’ alisema.