Tanzania yafanya vizuri katika Uwekezaji


TANZANIA imeelezewa kufanya vizuri katika sekta ya uwekezaji kwa kuwa na uwiano wa zaidi ya asilimia 30 katika ukuaji wa pato la ndani (GDP) katika kipindi cha mwaka 2008 licha ya dunia kukabiliwa na mdororo wa kiuchumi ukilinganisha na asilimia 23 ya nchi zinazoendelea (LCD)

Hayo yalisemwa leo na Mshauri wa Masuala ya Uchumi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa ( UNDP) nchini, Bw. Amarakoon Bandara wakati alipokuwa akitoa ripoti ya mkutano wa nchi zinazoendelea unahusu masuala ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD) kwa mwaka huu kwa waandishi wa habari.

Ripoti hiyo inahusisha nchi 49 zinazoendelea ikiwemo Tanzania, imehusisha sekta za uchumi, kilimo, fedha, mabadiliko ya hali ya hewa, Biashara, na umasikini.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2000 hadi 2007 uchumi wa nchi hizo ulikua kwa wastani wa asilimia saba kwa mwaka, lakini kati nchi, mataifa 14 uchumi wake ulianguka au kupanda kwa kiwango cha polepole.

Aidha Bandara alisema gharama za uigizaji wa chakula kutoka nje ya nchi ziliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni tisa hadi bilioni 24 katika kipindi hicho.

“Haya yote yanasababisha harakati za ukuaji wa maendeleo kwa sasa kukwama, hivyo katika kipindi hicho upunguzaji wa watu wanaoishi kwenye kipato cha chini ulikuwa mdogo .Nchi masikini zinatakiwa kujenga uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye thamani ili kuweza kukabiliana na tatizo hili,” alisema Bandara.

Kwa mujibu wa Bandara alisema ripoti hiyo inaonyesha kuwa idadi ya watu wanaoishi katika hali ya masikini(kipato kidogo) imeongezeka kwa zaidi ya milioni tatu kwa mwaka katika kipindi hicho. Wakati Tanzania idadi hiyo ilikuwa ni milioni 1.3 katika kipindi cha ukuaji huo.

Akifafanua zaidi Bandara aliongeza kuwa sekta ya uzalishaji wa bidhaa ulisimama katika kipindi cha mdororo wa kiuchumi cha mwaka 2000 hadi 2007, kwa asilimia 10 ya GDP, nchi 27 zilikumbwa na hali ya kuzorota kwa ukuaji wa viwanda katika kipindi hicho. Pia uzalishaji wa bidhaa zenye thamani ulikuwa chini licha ya kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao.

Naye Ofisa Mshauri wa Uchumi wa UNCTAD kwa Afrika, Junior Davis alisema nusu ya idadi ya nchi za LCD ziko katika hatua nzuri kufikia malengo ya Milenia (MDG’s) katika uandikishaji ya wanafuzi ya shule ya msingi, huku theluthi moja ya nchi hizo zikiwa zimefikia lengo la kuwapatia watu wake maji safi na salama wakati robo ya nchi hizo ziko kwenye hatua nzuri ya kupunguza idadi ya vifo watoto wachanga na watoto.

Msaidizi wa Mwakilishi wa UNDP, Ernest Salla alisema nchi za LCD zinatakiwa kuimarisha uhusiano na nchi zilizoendelea ili kuweza kukabiliana na matatizo hayo