Na Janeth Mushi, Arusha
TANZANIA imefanikiwa kudhibiti kemikali zinaharibu hewa ya tabaka la Ozoni kwa kupiga marufuku kemikali hizo kwenye majokofu, viyoyozi vya magari na baadhi ya vipodozi. Taarifa hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Raymond Mushi, alipokuwa akifungua mkutano wa wadau anuai wa masuala ya mazingira nchini.
Mkuu huyo wa wilaya alisema Tanzania imeweza kudhibiti matumizi hayo ya kemikali ambapo yamepungua kutoka tani 36.2 mwaka 2010, ukilinganishwa na tani 254 mwaka 1999 ikiwa ni sawa na asilimia 86.
Alisema lengo la mkutano huo ni kujadili taarifa za utekelezaji wa
mikataba ya Vienna na Montreal, Sheria ya Usimamizi wa Kanuni za
Mazingira pamoja na mchango wa sekta ya majokofu na viyoyozi katika
kulinda tabaka la Ozoni.
Aidha ameongeza kuwa siku ya Ozoni yenye kauli mbinu “Uondoshaji wa
Matumizi ya gesi za HCFC na Mchango muhimu katika kulinda tabaka la
Ozoni na kuzuia mabadiliko ya Tabia Nchi” imeamua kusherekewa kwa
kutoa mafunzo kwa wadau anuai juu ya kulinda mazingira.
Amesema hatua za utunzaji wa mazingira zisipochukuliwa ikiwemo utunzaji wa tabaka, hali hiyo inaweza kusababisha madhara kwa watoto ongezeko la magonjwa ya saratani na mtoto wa jicho.
Mushi alisema udhibiti huo wa kemikali umetokana na wadau wa mazingira kusimamia sheria mbalimbali za ulindaji wa mazingira pamoja na wahusika kutoka Mamlaka ya Ukusanyaji Mapato (TRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Vyuo mbalimbali vya Ufundi Stadi pamoja na wananchi ambao wanapewa elimu juu ya kulinda tabaka hilo la Ozoni.
“Hivi sasa juhudi zaidi zinahitajika pamoja na uzalendo wa kulinda
hewa hiyo isiweze kupotea kwa wahusika wa TRA au TBS kuacha tamaa za kupitisha mizigo ambayo inaonyesha wazi kuwa ni hatari kwa matumizi ya binadamu pamoja na mazingira”alisisitiza Mkuu huyo.
Kwa upande wake Ofisa Mfawidhi kutoka Shirika la Viwango Tanzania
(TBS), Deonard Manyanga ambaye anafanya kazi katika mpaka wa Namanga alisema baadhi ya kemikali haribifu ambazo ni R11 na R12 zimepewa muda hadi kufikia mwaka 2012 zitakuwa zimekwisha kwa sababu ya kutokubaliwa kuingizwa tena nchini.
Manyanga alisema kemikali R134 A na R 600 A ambazo zitakuwa kama
nembo kwenye majokofu, viyoyozi vya nyumbani na kwenye magari na
kuongeza kuwa kadri muda unavyozidi kwenda kila kitu kitakachoingizwa nchini kitaweza kuwa na nembo ambayo mhusika wa ukaguzi atagundua ni kemikali gani ambayo haitaweza kuleta madhara kwa binadamu pamoja na kuharibu mazingira.