RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono kwa dhati jitihada za Zimbabwe katika kutafuta mwafaka wa kudumu wa kisiasa na daima itaendelea kushikamana na wananchi wa Zimbabwe katika jitihada hizo.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Ijumaa, Mei 25, 2012, wakati alipompokea na kuzungumza na Mjumbe Maalum wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kwenye Ikulu Ndogo mjini Dodoma ambako Rais Kikwete anashiriki katika Semina Elekezi kwa ajili ya Wakuu wa Mikoa, Maafisa Tawala wa Mikoa na Wakuu wapya wa Wilaya.
Mjumbe huyo maalum, Sydney Sekeremayi ambaye ni Waziri wa Nchi katika Serikali ya Rais Mugabe, yuko kwenye ziara ya kanda ya nchi Wanachama wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), kuwaelezea Wakuu wa Nchi za Jumuia hiyo maendeleo ya kisiasa nchini Zimbawe na utekelezaji wa Makubaliano ya Kisiasa ya Global Political Agreement (GPA) nchini humo.
Sekeremayi amemweleza Rais Kikwete kuhusu maendeleo ya utungaji Katiba mpya nchini humo ambayo Rasimu yake ya kwanza tayari imetangazwa na sasa inajadiliwa na wadau wakuu wanaounda GPA kabla ya kuwasilishwa kwenye Bunge la nchi hiyo.
Waziri huyo amemwelezea Rais Kikwete kuhusu baadhi ya maeneo makuu katika Katiba hiyo ikiwa ni pamoja na Mfumo wa Serikali, Usambazaji Madaraka kwa Wananchi, Suala la Uraia wa zaidi ya nchi moja na Uhuru wa Kijinsia.
Rais Kikwete ameipongeza Zimbabwe kwa kuendelea kutekeleza makubaliano ya GPA bila kuyumba pamoja na changamoto zote zinazokabili utekelezaji huo na kusema kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono kwa dhati jitihada za wananchi wa Zimbabwe kuleta mwafaka wa kisiasa nchini humo.
“Napenda kumhakikishia Rais Mugabe kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono kwa dhati jitihada za wananchi wa Zimbabwe kujenga mwafaka wa kudumu wa kisiasa. Daima tutaendelea kuwa upande wa wananchi wa Zimbabwe,” amesema Rais Kikwete na kusisitiza umuhimu wa mashauriano na maridhiano ya kisiasa ambayo husababisha utulivu wa msingi kabisa katika nchi yoyote kama ilivyotokea katika Tanzania Visiwani.
Rais pia amemweleza Sekeremayi kuhusu mchakato wa utunzi mpya wa Katiba katika Tanzania akisema: “Kama unavyojua na sisi tumeanzisha mchakato wetu wa kutunga Katiba mpya. Niliamua tuanzishe mchakato huo kwa sababu sikuona sababu yoyote ya Watanzania kuvutana bila sababu za msingi kuhusu suala la Katiba kwa sababu baadhi ya wananchi walikuwa wanaamini kuwa walikuwa wanashindwa kwenye uchaguzi kwa sababu ya Katiba ya sasa.”