TANZANIA na Uganda zimekubaliana kuharakisha ujenzi wa reli ya Tanga-Musoma-Uganda ili kuhitimisha ndoto ya miaka mingi ya Mwanzilishi wa Taifa la Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Nchi hizo mbili pia zimekubaliana kupanua bandari za Tanga na Musoma katika Tanzania, na kujenga bandari mpya nchini Uganda ili kuhudumia reli hiyo mpya kati ya nchi hizo mbili.
Hayo ndiyo yalikuwa maamuzi makuu yaliyofikiwa leo, Jumatatu, Oktoba 3, 2011, katika mkutano kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Rais Museveni ambaye amefanya ziara ya kikazi ya siku moja nchini Tanzania amewasili leo asubuhi na kupokea na mwenyeji wake Rais Kikwete kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam. Kiongozi huyo wa Uganda ameondoka kurejea nyumbani baada ya mazungumzo na mwenyeji wake.
Wakati wa mazungumzo yao, viongozi hao wawili wamekubaliana kuharakisha ujenzi wa reli hiyo kama njia ya kufungua mlango wa tatu wa Uganda kupitishia bidhaa zake kutoka na kwenda kwenye Bahari ya Hindi. Milango mingine inayotumiwa na Uganda kusafirisha bidhaa kutoka na kwenda Bahari ya Hindi ni bandari za Dar es Salaam na Mombasa, Kenya.
Katika kuhakikisha uamuzi wake wa kuharakisha ujenzi huo unaanza katika muda mfupi iwezekanavyo, viongozi hao wawili wameunda kikosikazi cha kusimamisha suala hilo. Kikosi kazi hicho kitaundwa na mawaziri wa wizara za usafirishaji na uchukuzi, fedha na mambo ya nje kwa kila nchi.
Chini ya mpango huo, bidhaa zitasafirishwa kwa reli kutoka Bandari ya Tanga hadi Bandari ya Musoma na kuwekwa kwenye pantoni maalum ya (wagon ferry) reli kutoka Bandari ya Musoma hadi bandari mpya ya Uganda kwa kuvushwa Ziwa Victoria.
Viongozi hao wamefanya uamuzi wa kuharakisha ujenzi huo kwa sababu ya faida za reli hiyo kwa chumi za nchi zote mbili lakini pia kwa kujua kuwa bila usimamizi wa karibu wa Tanzania na Uganda itachukua miaka mingi zaidi kwa reli hiyo kuweza kujengwa.
Wazo la kujenga reli ya kuunganisha Uganda na Bandari ya Tanga kupitia Bandari ya Musoma liliasisiwa miaka mingi tokea awamu ya kwanza ya uongozi wa Tanzania, lakini kwa namna moja ama nyingine, utekelezaji wa wazo hilo umekumbana na changamoto mbalimbali.
Katika mkutano wao wa leo, viongozi hao pia wamejadili masuala mengine yanayohusu uhusiano kati ya nchi hizo mbili na masuala mengine ya kikanda na kimataifa.