Tanzania, Oman Wakubaliana Kushirikiana Kiuchumi na Kisiasa

Moja ya miji ya Oman


Na Magreth Kinabo-MAELEZO

SERIKALI ya Tanzania na Oman zimeahidi kushirikiana katika masuala ya kiuchumi na kisiasa ikiwa hatua ya kuhimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili. Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe mara ya kutia saini mkataba wa makubaliano ya kisiasa (Political Consulatation Exchange) na Waziri anayeshughulikia masuala ya Mambo ya Nje wa Oman, Yousef bin Alawi bin Abdullah katika hafla fupi iliyofanyika kwenye hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro Kempsink, Dar es Salaam.

“Mkutano umeisha salama tumeweka makubaliano ya kutosha na watalaam maendeleo kwenye maeneo ya biashara, kilimo, miundombinu, bandari, reli, viwanda, madini, mafuta, gesi wanyama yaani nyama ya ngo’mbe itakuwa ikisafirishwa,” alisema Waziri Membe huku akisisitiza kuwa biashara ni uchumi hivyo lazima uchumi hukuzwe kwa ushirikiano kati ya nchi hizo.

Alisema maeneo hayo yalijadiliwa na kukubaliwa na pande zote mbili. Waziri Membe aliongeza kuwa wamekubaliana kuwa ofisi ya ushirikiano huo wa kiuchumi iwepo hapa nchini, ambapo serikali ya Oman itajenga jengo lake la uwekezaji hapa, ambalo litakuwa jijini Dares Salaam.

Kwa upande wake Waziri wa Abdullah alisema kutakuwepo na mikutano ya mara kwa mara kwa ajili ya kuangalia namna ya kutekeleza makubaliano hayo. Makukubaliano ya ushurikiano huo yametokana na ziara ya Rais Jakaya Kikwete aliyoifanya nchini Oman, Oktoba, mwaka jana.