Na Mwandishi Maalumu, Oman
TANZANIA na Oman zimetiliana saini mikataba mitano itakayoziwezesha nchi hizo kufanya biashara baina yake kwa uaminifu na utaratibu ambao unaridhisha pande zote. Mikataba hiyo imetiwa saini katika mkutano wa wafanyabiashara wa Oman tarehe 16 Oktoba, 2012 na kushuhudiwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Mikataba hiyo inahusu kuundwa kwa Baraza la Biashara baina ya Oman na Tanzania, kukuza na kulinda biashara, majadiliano ya kisiasa na, Elimu ya Juu na makubaliano ya utunzaji na uwekaji kumbukumbu. Mara baada ya kutiliana saini mikataba hiyo, Rais Kikwete amewaeleza wafanyibiashara wa Oman kuwa Tanzania iko tayari kufanya biashara na Oman na kwamba milango iko wazi, hivyo kuwakaribisha wale wote wenye nia na uwezo wa kuwekeza katika Kilimo, Viwanda,Uvivu, Utalii na Sekta mbalimbali ambazo Tanzania imejaliwa kuwa nazo.
Rais amesema mbali na Tanzania kuwa na eneo kubwa ambalo linajumlisha Bara na Visiwani, “Tanzania ni mlango mkuu kwa nchi za Afrika Mashariki na pia zile zilizopo kusini mwa Afrika na Maziwa Makuu” amesema. Na kuwaasa wafanyibiashara wa Oman kuja kuwekeza Tanzania.
Mapema kabla ya Rais kufungua rasmi mkutano wa wafanyabiashara, Mwenyekiti wa Chama cha wafanyabiashara na wenye Viwanda cha Oman, Khalil Al Khonji ameelezea jinsi nchi mbili hizi zinavyofurahia na kuuenzi uhusiano wa kindugu baina yake.
“Mahusiano ya karibu baina ya Oman na Tanzania yanaenziwa na serikali pamoja na wananchi wake, na tunapoongelea kukuza biashara na uwekezaji kwa ajili ya nchi zetu, tunategemea kupata suluhisho la kudumu la kuondokana na tatizo la kutokuwepo kwa uwekezaji katika nchi zetu” amesisitiza.
Mapema kabla ya kufungua mkutano wa wafanyabiashara, Rais Kikwete ametembelea makumbusho ya kijeshi Bait Al Falaj ambapo ameelezwa historia ya nchi ya Oman. Rais pia ameweka jiwe la msingi ambapo utajengwa ubalozi wa Tanzania nchini Oman.
Katika siku yake hii ya pili, Rais Kikwete amealikwa kwenye chakula cha usiku na Sultani Qaboos Bin Said. Rais anaendelea na ziara yake ambapo anatarajiwa pia kukutana na watanzania wanaoishi na kufanya kazi Oman.