Na Frank Mvungi – Maelezo
MAKAMU wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wakati wa mkutano Mkuu wa Taasisi za Kodi Afrika (Africa Tax Admistration forum-ATAF) utakaowahusisha wataalamu wa masuala ya Kodi kutoka Sehemu mbalimbali Duniani. Mkutano huo unatarajiwakufanyika kuanzia septemba 16mwaka huu katika Hotel ya Double Tree jijini Dar es salaam.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es salaam na Kamishana Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Rished Bade wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
“Lengo la mkutano huu ni kujadili namna ya kuimarisha taasisi za Kodi Africa na kuwajengea uwezo watumishi katika taasisi za kodi,” alisema Bade.
Akifafanua Bade amesema ATAF ni chombo cha Kimataifa kinachotambuliwa na jumuiya za Kimataifa kinachojihusisha na masuala ya kodi ambapo Tanzania itanufaika na mkutano huo kwa kupata fursa ya kujitangaza Kimataifa. Katika kuzijengea uwezo nchi za Afrika Bade amesema ATAF inalenga kuboresha Mamlaka za Mapato lengo likiwa ni kukuza mapato ya ndani yatokanayo na kodi.
Akitaja baadhi ya mada zitakazo wasilishwa Bade alisema kuwa ni pamoja na Uongozi katika Agenda ya Kodi Kimataifa na taswira ya Taasisi za Kodi Afrika. Pia Bade alisema kuwa wataalamu wa Kodi watabadilishana uzoefu wa kukusanya kodi katika sekta mbalimbali pamoja na kubadilishana taarifa muhimu za biashara za kimataifa na uwekezaji katika nchi za Afrika.
Tanzania imekuwa mwanachama wa ATAF tangu mwaka 2009 ambapo nchi wanachama ni Benin, Botswana, Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Chad, Comoros, Egypt, Eritrea, Gabon, Gambia, Ghana. Nchi nyingine ni Ivorycoast, Kenya, Lesotho, Liberia, Madagasca, Malawi, Mauritania, Mauritius, Morocco, Mozambique, Namibia, Nigeria, Rwanda, Senegal, Seychelles, Sierra leone, South Afrika, Sudan, Uganda, Zambia na Zimbabwe na Tanzania.