TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MASHINDANO YA SHIRIKISHO LA MICHEZO YA SHULE ZA SEKONDARI AFRIKA MASHARIKI
Tanzania imepewa heshima ya kuwa Mwenyeji wa mashindano ya Michezo ya shule za Sekondari Afrika Mashariki yajulikanayo kama FEASSSA (Federation of East Africa Secondary Schools Sports Association),ambayo yatafanyika Jijini Dar es salaam kuanzia tarehe 22 Agosti hadi 1 septemba mwaka huu 2014.
Wanachama wa mashindano haya ni Wanafunzi wa shule za sekondari kutoka Wizara zenye dhamana ya elimu katika nchi wanachama wa Jumiya ya Afrika Mashariki. Nchi hizo ni:-
NO. NCHI WACHEZAJI VIONGOZI JUMLA
WASICHANA WAVULANA
1. Tanzania Bara 310 270 120 700
2. Tanzania Zanzibar 34 70 15 119
3. Uganda 422 393 89 904
4. Rwanda 129 142 79 350
5. Kenya 327 326 88 741
6. South Sudan 215
7. Burundi 208 41 249
JUMLA 3,178
Michezo hii mikubwa katika Ukanda huu,inategemewa kukutanisha Wanamichezo zaidi ya 3000 (elfu tatu) watakaoshiriki michezo ifuatayo:-
1. Mpira wa Miguu-Wavulana na Wasichana
2. Mpira wa Kikapu-Wavulana na Wasichana
3. Mpira wa Wavu-Wavulana na Wasichana
4. Mpira wa Mikono-Wavulana na Wasichana
5. Netiboli-Wasichana
6. Mpira wa Meza –Wavulana na Wasichana
7. Riadha-Wavulana na wasichana
8. Mpira wa Magongo (Hockey)-Wavulana na Wasichana
9. Lawn tennis- Wavulana na wasichana
10. Badminton-Wavulana na Wasichana
11. Rugby-Wavulana
12. Kuogelea-Wavulana na Wasichana
Madhumuni ya FEASSSA ni kufanya mashindano ya michezo kwa Wanafunzi wa shule za Sekondari kwa Nchi wanachama kwa malengo ya kujenga mahusiano, ushirikiano, mshikamano, upendo na umoja miongoni mwa vijana na raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kilele hiki hutoa taswira ya chachu ya Michezo shuleni na maandaalizi ya timu za Taifa za Vijana katika uwakilishi wa nchi zao.
Mashindano yameendelea kufanyika kila mwaka tangu 2002, kwa mara ya kwanza yalifanyika Nairobi nchini Kenya. Nchi Mwenyeji huteuliwa na Kamati ya utendaji ya FEASSSA kwa kuangalia kukidhi vigezo vya uenyeji. Tanzania ilikuwa Mwenyeji kwa mara ya mwisho 2006 Dar es salaam.
Viongozi mbali mbali kutoka nchi wanachama, wataambatana na Wanamichezo wao kushiriki shughuli hii muhimu na kutoa fursa zingine kama za kibiashara, kielimu, kiutamaduni na kiutalii kwa faida na manufaa ya wananchi wetu.Ni fursa nzuri pia kuona ushirikiano wa Wizara zetu kama ya Uhusiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Habari, Vijana ,Utamaduni na Michezo nk. katika kuleta ufanisi wa Uenyeji huu.
Aidha, viwanja vitakavyotumika katika michezo hii ni pamoja na:-
• Uwanja wa Taifa ambapo licha ya kutumika kwa ufunguzi na ufungaji wa mashindano, michezo ya netiboli, mpira wa kikono, mpira wa wavu, mpira wa kikapu, mpira wa na tennis itachezwa kwenye viwanja vilivyochorwa kuzunguka eneo la uwanja huo
• Viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam kwa michezo ya ruby, hockey na kuogelea
• Viwanja vya Chuo cha Polisi kwa ajili ya mpira wa miguu
• Jitegemee Sekondari viwanja vya mazoezi
• Viwanja vya Twalipo
• Uwanja ndani kwa ajili badminton
• Uwanja wa karume mpira wa miguu
• DUCE mpira wa miguu
Shule za Tanzania zinazoshiriki mashindano hayo ni zile zilizofanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali yaliyofanyika hapa nchini ambazo ni:-
• Makongo Sekondari ya Mkoa wa DSM
• Lord Baden Powell ya Mkoa wa Pwani
• Tirav Sekondari ya Mkoa wa DSM
• Kilabela Sekondari ya Mwanza
• Techford Sekondari ya Morogoro
• Kizuka Sekondari ya Morogoro
• Abdul Jumbe sekondari, Kigamboni DSM
• Shule ya Wasichana Masasi , Mtwara
• Popatlali Sekondari Tanga
• Tanga Sekondari
• Meliwa Sekondari, Dodoma
• Iyunga Sekondari
Mashindano haya yatafunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 24/08/2014 saa 8.00 mchana na kufungwa rasmi na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dk. Mohammed Shen tarehe 31/ 08/2014 saa 8.00 Uwanja wa Taifa na viongozi wa juu katika Taifa letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamealikwa kushiriki katika hafla hizo.
Vile vile mabalozi wa nchi zinazoshiriki michezo hiyo wamealikwa kushiriki ufunguzi, ufungaji na kuwa wageni wa heshima wakati wote wa mashindano hayo.
Tahadhari zote za ulinzi na usalama wa watu na mali zimewekwa kupitia vikao mkakati ambapo jeshi la polisi na usalama vimetoeushirikiano katika vikao kazi vyote tulivyokaa kwa ajili ya kufanikisha mashindano haya. Hivyo, wananchi mnaomba kujitokeza kwa wingi kuja kushuhudia na kushangilia timu zetu na vilevile kutia hamasa ya michezo hii.
Timu za kutoka nje ya Tanzania zinatarajiwa kuwasili tarehe 22/08/2014 kupitia Mtukula, Lusumo, Kakongo na Namanga. Timu zote zitakapowasili Tanzania zitapumzika katika shule za Bishop Durning sekondari ya Arusha na Mwenge Sekondari ya Singida.
Washindi wa michezo hiyo watatunukiwa zawadi mbalimbali zikiwemo Medali na vikombe. Timu yetu ya Tanzania imeweka kambi ya wiki moja katika Chuo Kikuu Kishiriki cha DUCE.
Tunatoa wito kwa watanzani wote na wapenda Maendeleo ya michezo kuona umuhimu wa kuisaidia timu hii ili iweze kufanya vizuri zaidi katika mashindano haya.
KARIBUNI WOTE MTUUNGE MKONO KUFANIKISHA TUKIO HILI KUBWA NA LA AINA YAKE.