Na Tiganya Vicent, MAELEZO
JUMLA ya sh. milioni 400 zinatarajiwa kutumika kugharamia shughuli za uendeshaji wa sensa ya majaribio itakayofanyika Septemba 4 hadi 11 mwaka huu katika mikoa 11 ya Tanzania.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Morogoro na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk. Albina Chuwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye mafunzo ya wiki moja ya wakufunzi wa sensa ya majaribio yanayofanyika mjini hapa.
Alisema kuwa Sensa ya majaribio itakayofanyika Septemba 4, mwaka huu ni sehemu ya maandalizi ya maandalizi ya sensa kuu ya watu na makazi ya mwaka 2012.
Akizungumza mafunzo ya wakufunzi wa sensa ya majaribio Dk. Chuwa, alisema kutokana na umuhimu wa sensa ya watu na makazi Ofisi yake imedhamiria kuboresha zoezi hilo la Sensa ya majaribio ili kuweza kurekebisha kasoro zinazoweza kujitokeza hapo baadae.
Dk. Chuwa aliongeza kuwa wameamua kutumia fedha ili kubana matumizi ya fedha za serikali na ndiyo maana wamechukua mikoa michache kwa ajili ya kufanya sensa ya majaribio na kuwaomba watanzania watambue umuhimu wa zoezi hili kuanzia sasa wajiandae kwa kuhesabiwa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Alisema katika sensa ya majaribio jumla ya kaya 5000 zitahojiwa kwa ajili ya kupata taarifa zao muhimu ambazo zitaingizwa katika kumbukumbu za NBS.
Dk. Chuwa alisema kutokana na hali hiyo NBS itatoa mafunzo kwa watu wapatao 100, 000 kwa ajili ya kukusanya taarifa kwa namna itakayokidhi vigezo na mfumo thabiti wa mafunzo kwa watalaamu wake.
Naye Meneja wa sensa ya watu na makazi wa NBS Irenius Ruyobya alisema kuwa mara baada ya kukamilika kwa sensa ya majaribio wanatarajia kukutana na wadau mbalimbali mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu kwa ajili kujadili changamoto zilizojitokeza na kuboresha kwa ajili ya sensa ya mwakani.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Amina Mrisho, alisema kwa kutambua muhimu wa sensa serikali imejipanga kikamilifu ili kuhakikisha sensa ya watu na makazi inafanikiwa kwa ubora wa hali ya juu ili kwenda sambamba na mafanikio ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania.
Alisema kuwa lengo la sensa ya watu na makazi ni kuiwezesja serikali na jamii kwa ujumla kuweka misingi ya kutunga sera ambazo zinatafanikisha maendeleo kwa Taifa na awatu wake.