Tanzania imetangaza kuisaidia Somalia kwa kutoa msaada wa tani 300 za mahindi, ili kuwasaidia kupunguza makali ya ukosefu mkubwa wa chakula unaowakabili kiasi cha wananchi milioni 3.5 wa Jamhuri hiyo
Tanzania pia imeahidi kutoa misaada mingine kwa nchi hiyo kwa kadri uwezo wa nchi unavyoruhusu katika kuisaidia Somalia kukabiliana na matatizo makubwa ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiusalama ambayo yamekuwa yanaikabili nchi hiyo mfululizo katika miaka 20 iliyopita.
Mchango wa Tanzania umetangazwa wakati wa mazungumzo rasmi kati ya Serikali ya Tanzania na ile ya Jamhuri ya Somalia, na wakati wa futari ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, amemwandalia mgeni wake Rais wa Somalia, Mheshimiwa Sheikh Sharif Sheikh Ahmed ambayo yuko katika ziara ya siku mbili ya kikazi nchini
“Tunasikitika sana kuona matatizo makubwa ya ukosefu mkubwa wa chakula yanayoikabili nchi yako. Kama unavyojua Tanzania ni nchi masikini na uwezo wetu siyo mkubwa. Lakini tuna methali hapa isemayo kutoa ni moyo siyo utajiri. Kwa hiyo kwa moyo huo wa mtu masikini, tumeamua kutoa mchango wetu mdogo wa tani 300 za mahindi ambazo ni sawa na magunia 3,000 ili kusaidia ndugu zetu wa Somalia kukabiliana na hali ya njaa kubwa,” Rais Kikwete amemwambia Rais Sheikh Ahmed.
Ameongeza Rais Kikwete: “Tunajua kuwa mahitaji yenu ni makubwa zaidi kuliko hiki kidogo tulichotoa. Lakini sasa ndiyo kwanza tumeingia katika msimu wa mavuno. Tutaangalia huko mbele kama tunaweza kuwachangia zaidi ndugu zetu wa Somalia.
“Tunazungumza pia na marafiki zetu ili tuwashawishi kuona kama nao wanaweza kuunga mkono jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Somalia ya kuhakikisha inapata chakula cha kutosha ili kuokoa maisha ya mamilioni ya wananchi.”
Wakati wa futari ambayo Rais Kikwete amemwandalia Rais huyo wa Somalia katika Mwezi Mtukufu huu wa Ramadhani, Rais Kikwete ametoa mwito kwa makampuni yanayotengeza maji nchini kusaidia kuchangia upatikanaji wa maji kwa wananchi hao wa Somalia. Somalia inahitaji mamilioni ya lita za maji ili kukabiliana na ukosefu mkubwa wa chakula na maji.
“Tutazungumza na makampuni yanayotengeneza maji hapa nchini kama nayo yanaweza kuchangia kupambana na janga hili kubwa linalowakabili wananchi wa Somalia,” Rais Kikwete amemwambia Rais wa Somalia katika shughuli ya futari.
Shughuli hiyo imehudhuriwa na watu wengi wakiwamo mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Tanzania, wakuu wa mashirika ya umma na binafsi nchini, mawaziri, makatibu wakuu na maofisa waandamizi wa Serikali na mawaziri wakuu wa zamani, Mzee Salim Ahmed Salim na Mzee Joseph Warioba.
Katika mazungumzo hayo rasmi, Tanzania na Somalia, zimezungumza masuala mengi ambako nchi hizo zinaweza kushirikiana kuisaidia Somalia baada ya ujumbe wa nchi hiyo kuelezea maeneo ambako Tanzania inaweza kuisaidia Somalia kama katika mapambano ya pamoja dhidi ya ugaidi katika Bahari ya Hindi na kusaidia kufundisha wataalam wa fani mbalimbali.
Rais Kikwete pia amempongeza Rais wa Somalia na ujumbe wake wa mafanikio ya kijeshi dhidi ya kikundi cha kigaidi cha El Shabaab ambacho kimefukuzwa katika maeneo mengi ya mji mkuu wa Mogadishu ambayo kimekuwa kinayashikilia kwa muda mrefu.
Rais pia amempongeza Rais Sheikh Sharif Sheikh Ahmed kwa mafanikio yake mengine ya kuleta utulivu zaidi ndani ya Serikali yake na kuongeza muda wa utumishi wa Serikali na Bunge kama moja ya njia ya kuleta maelewano ndani ya Serikali, na kati ya Serikali na Bunge la nchi hiyo.