Tanzania kushirikiana kupambana na uharamia

Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu

Na Joyce Ngowi

WAZIRI wa Uchukuzi, Omari Nundu amesema Tanzania itashirikiana na nchi nyingine zinazotumia huduma ya usafirishaji kwa njia ya bahari kupambana na vitendo vya uharamia ili kudhibiti hali hiyo.

Waziri Nundu alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa Maofisa wa Ngazi za Juu kuhusu makubaliano ya kupambana na uharamia na uhalifu vyombo vya usafirishaji Magharibi mwa Bahari ya Hindi na Ghuba ya Aden.

Katika mkutano huo ulio hudhuriwa na Viongozi kutoka nchi 22 za ukanda ambao vitendo vya uharamia vinafanyika, Waziri Nundu alisema vitendo vya kiharamia licha ya kuharibu usalama wa meli na mazingira na binadamu pia vimekuwa vikipoteza fedha nyingi.
Alisema tathimini ya One Earth Future Foundation kuhusu gharama za kiuchumi inakadiriwa kuwa uharamia wa Somalia uligharimu kati ya Dola za Marekani 6.6 hadi 6.9 mwaka jana, ambayo ilihusisha gharama za kukomboa meli watu na vitu vilivyo kuwemo.

“Tupo tayari kushirikiana na nchi nyingine katika ukanda huu pamoja na washiriki wengine kupiga vita dhidi ya uharamia eneo la Magharibi mwa Bahari ya Hindi na Ghuba ya Aden,” alisema Nundu.

Alibainisha kuwa uharamia kwenye mwambao wa Somalia umetishia safari za meli kuanzia mwanzo wa vita ya wao kwa wao, mwaka 1990.

Naye Katibu Mkuu kutoka Shirika la Bahari Duniani (IMO), Hartmut Hese alisema katika mkutano huo wa siku mbili watajadili juu ya kupambana na vita dhidi ya uharamia ambayo imeonekana kuwa changamoto kubwa.