Na Mwandishi Wetu
TANZANIA inaungana na nchi nyingine mbalimbali duniani kuadhimisha miaka 67 ya Umoja wa Mataifa ambapo kutakuwa na shughuli anuai zinazoanza leo Oktoba 17 hadi 24, 2012 ambayo ndio siku ya kilele cha shughuli hizo.
Kitaifa nchini Tanzania miaka 67 ya Umoja wa Mataifa itaadhimishwa kwa kauli mbiu ambazo zimekuwa zikitoka kila mwaka na kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Changing Peoples’ Lives: Greening The Environment For Sustainable Livelihoods’.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule amesema kauli mbiu hiyo imekuja wakati muafaka ili kutukumbusha mahusiano yetu ndani ya Jumuiya ya Umoja wa Mataifa lakini vilevile inatukumbusha changamoto ya jinsi uharibifu wa mazingira unavyofanyika hivi sasa.
Ameongeza kuwa wiki ya maadhimisho ya miaka 67 ya Umoja wa Mataifa itaadhimishwa na matukio mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa leo, na Siku ya Familia itakayohusisha michezo mbalimbali itakayofanyika kwenye viwanja wa Leaders Club Oktoba 20, 2012.
Michezo hiyo itawahusisha wanadiplomasia waliopo nchini Tanzania, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje.