TANZANIA KUONGOZA NCHI ZA AFRIKA KATIKA MABORESHO YA UTOAJI HAKI ZA WATUHUMIWA NA MAHABUSU
Utekelezaji wa miongozo ya Luanda kuimarisha haki za binadamu nchini
UTEKELEZAJI wa Miongozo ya Luanda (Luanda Guidelines) kuhusu ukamataji na ushikiliaji wa watuhumiwa kabla ya kufunguliwa mashtaka utakaoanza hivi karibuni unatarajiwa kuimarisha haki za watuhumiwa na mahabusu nchini.
Aidha, miongozo hiyo inatarajiwa kuipunguzia Serikali mzigo mkubwa wa gharama za uendeshaji wa mahabusu na magereza ambayo mengi yao yana msongamano mkubwa wa watuhumiwa na wafungwa.
Kutokana na tafiti zilizofanyika barani Afrika ikiwemo Tanzania imebainika kuwa, kuna uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu kwenye mchakato mzima wa mfumo wa haki–jinai (criminal justice) ambao unaanzia pale mtu anapokamatwa na vyombo vya dola (arrest), wakati wa mahojiano (interrogation) na hata anapokuwa mahabusu katika vituo vya polisi na magerezani.
Kwa mujibu wa taarifa za kiutafiti, wengi wao wanakamatwa pasipo utaratibu, kudhalilishwa, kuteswa, kubambikiwa kesi, kuwekwa muda mrefu bila kufikishwa mahakamani na kuwepo mazingira magumu ya dhamana jambo linalokiuka haki za binadamu zilizoainishwa katika Ibara ya 12 mpaka 24 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, sheria nyinginezo za nchi pamoja na Mikataba ya Kimataifa ambayo nchi imeridhia.
Miongozo hii inatanabaisha namna binadamu walioko katika hali na mazingira tajwa wanapaswa kuangaliwa kulingana na taratibu, kanuni na sheria zenye vigezo na viwango vya kitaifa na kimataifa kuhusu haki za binadamu.
Miongozo hii inahimiza uzingatiaji wa haki za binadamu katika mfumo wa haki-jinai – yaani katika hatua ya ukamataji na uhifadhi wa watuhumiwa wa uhalifu kabla hawajafikishwa mahakamani (Arrest and Pre-Trial detention) kama vile mahabusu za polisi na magereza
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti uliofanywa hivi karibuni na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa kushirikiana na Mtandao wa wataalamu wa masuala ya kipolisi kutoka taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali Afrika (African Policing Civilian Oversight Forum – APCOF) yenye makao yake makuu nchini Afrika Kusini asilimia 50 ya watu wanaoshikiliwa maeneo mbalimbali nchini ni mahabusu ambao, ama wanasubiri kufikishwa mahakamani au kesi zao bado zinaendelea katika mahakama mbalimbali (yaani hawajahukumiwa). Hali hii inaisababishia Serikali gharama kubwa za uendeshaji wa taasisi hizo.
Kuanza kutekelezwa kwa Miongozo hii ya Luanda kutaipunguzia Serikali gharama za uendeshaji kutokana na kupungua kwa idadi ya watu watakaokuwa wakishikiliwa vizuizini kwa kuwa wengi wengi wao wanashikiliwa kwa makosa ambayo yana dhamana (bailable offences) yakiwemo makosa madogo madogo kama vile wizi mdogo mdogo na kadhalika
Athari za watu kushikiliwa vizuizini pasipo ulazima ni pamoja na Serikali kuendelea kubeba mzigo mkubwa wa gharama za uendeshaji, watuhumiwa wa uhalifu (mahabusu) kupata magonjwa ya kuambukizwa kutokana na msongamano, kupata ulemavu na hata kufariki kutokana na mateso pale ambapo watumishi wa vyombo vya dola wanapotumia nguvu kupita kiasi wakati wa ukamataji na mahojiano.
Athari za kiuchumi ni pamoja na familia nyingi huathirika kwa kukosa mahitaji muhimu kama vile chakula, elimu kwa watoto, matibabu n.k kutokana na watafutaji (breadwinners) kushikiliwa vizuizini kwa muda mrefu.
Matatizo yaliyopo
Ukamataji unaofanywa na vyombo vya dola hususan jeshi la polisi mara nyingi unakiuka haki za binadamu kwani tafiti zinaonyesha kwamba kumekuwepo na matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya watuhumiwa, ambapo huambatana na vitendo vya utesaji wa watuhumiwa. Utesaji huo hufanywa wakati wa mahojiano (interrogation) kwa lengo la kuwashinikiza watuhumiwa kukiri makosa. Takwimu za tafiti zilizofanywa na Tume nyakati tofauti zinaonyesha pia kwamba yapo malalamiko mengi yanayopokelewa kutoka kwa watuhumiwa na wafungwa wanaolalamikia kubambikiwa kesi na polisi.
Aidha, kuna mapungufu katika mfumo wa sheria za jinai nchini Tanzania. Mathalani, ingawa Ibara ya 13(6)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 inakataza utesaji kwa watuhumiwa na kuelekeza mamlaka za nchi kutunga sheria kwa minajili hiyo, bado kuna upungufu katika sheria kwani Kifungu cha 29 cha Sheria ya Ushahidi, Sura ya 6 ya Sheria za Tanzania kinakataza ushahidi uliopatikana kwa shinikizo la aina yoyote kutumika kama ushahidi halali mbele ya mahakama.
Hivyo, mapungufu yanayojitokeza ni kwamba Sheria za nchi zinakataza vitendo vya utesaji kwa watuhumiwa wa uhalifu lakini hazitamki wazi ni hatua gani zitachukuliwa dhidi ya mtumishi wa chombo cha dola ambaye atajihusisha na vitendo vya utesaji wa watuhumiwa. Nafuu (remedy) pekee ya kisheria inayopatikana ni muathirika (victim) kufungua kesi ya madai dhidi ya serikali. Kwa upande mwingine, Sheria ya Kukazia Haki na Wajibu (Basic Rights and Duties Enforcement Act) ya mwaka 1994 nayo pia changamoto kwani ili kesi inahyohusu ukiukwaji wa haki za binadamu isikilizwe, linahitajika jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu. Katika mazingira ya sasa, upatikanaji wa jopo hilo ni mgumu kutokana na upungufu wa maji.
Tatizo jingine kubwa katika ukamataji, ushikiliaji watuhumiwa vituo vya polisi na kabla ya kesi kusikilizwa ni uelewa mdogo wa sheria, kanuni na taratibu zinazohusiana na haki za binadamu katika mfumo wa haki-jinai.
Kufuatia matatizo yaliyobainishwa hapo juu (matatizo katika ukamataji na ushikiliaji wa watuhumiwa katika mahabusu zilizoko katika vituo vya polisi na sehemu nyingine wanamoshikiliwa watuhumiwa kabla ya kushtakiwa), Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (African Commission on Human and Peoples Rights – ACHPR) ilianzisha mchakato wa kuandaa Miongozo (Guidelines) ya namna ya kukuza na kulinda haki za binadamu nyakati za kukamatwa kwa watuhumiwa, kuwekwa ndani ya selo za polisi na wakiwa mahabusu za magereza.
Miongozo hii iliridhiwa katika Mkutano Mkuu wa 55 wa Tume hiyo uliofanyika Luanda, Angola Mei, 2014 na hivyo kujulikana kama “Luanda Guidelines.” Luanda Guideline ziliandaliwa kwa mujibu wa Ibara ya 45(1)(b) ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (African Charter on Human and People Rights) wa mwaka 1981.
Aidha, katika kutekeleza jukumu tajwa na mchakato uliopitishwa na ACHPR, Miongozo imeanza kufanyiwa kazi kwa kuitambulisha kwa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (AU) ili kuijua na kisha kurekebisha taratibu, kanuni na sheria za jinai za nchi husika ili ziendane na miongozo tajwa.
Tanzania ni miongoni mwa nchi tano (5) za mwanzo Afrika zilizopewa kipaumbele katika utekelezaji wa miongozo hiyo ambayo itapelekea maboresho ya mfumo wake wa haki-jinai. Nchi nyingine zilizopewa kipaumbele sambamba na Tanzania ni Zimbabwe, Malawi, Tunisia na Ivory Coast.
Mwelekeo
THBUB kwa kushirikiana na African Policing Civilian Oversight Forum – APCOF, Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (ACHPR) pamoja na wadau wengine ndani ya serikali na asasi zisizo za serikali imeanza mchakato wa kuhamasisha utekelezaji wa Luanda Guidelinehapa nchini. Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Ofisi ya Kanda ya Afrika ndilo linalofadhili mchakato huu kwa sasa.
Mchakato bado upo katika hatua za awali ikiwa ni pamoja na kuandaa Mpango-Kazi wa Utekelezaji, kubaini taasisi zitakazo husika na utekelezaji huo na muda wa utekelezaji waLuanda Guidelines.
Hata hivyo, zoezi la kutambulisha miongozo hii limekwishaanza tangu mwishoni mwa mwezi uliopita kwa warsha iliyowashirikisha wadau mbalimbali wa hapa nchini. Katika warsha hiyo ya siku mbili wadau walipata fursa ya kutoa mawazo yao juu ya Mpango-Kazi wa Utekelezaji wa miongozo hii. Na kwa kupitia kwenu tunatarajia wadau na wananchi wengi zaidi watapata taarifa juu ya miongozo hii – tunaomba ushirikiano wenu.
Hatua zitakazofuata hapo baadaye zitajumuisha kufanya mapitio ya sheria za jinai zinazohusiana na ukamataji na ushikiliaji wa watuhumiwa na kubainisha mapungufu yaliyomo na kisha kuzifanyia marekebisho sheria hizo ili zikidhi viwango vilivyoainishwa katika Luanda Guidelines.
Pale ambapo mapungufu yatabainika kuwepo katika utekelezaji, sheria zitungwe au kurekebishwa ili kuwabana watendaji wa vyombo vya dola wanaokiuka sheria na miongozo ya kazi zao.
Kwa ujumla utekelezaji wa dhati wa sheria zilizopo au zitakazofanyiwa marekebisho au zitakazotungwa upya utasaidia kuimarisha utawala wa sheria, utu wa mtu, uhuru binafsi wa mtu, amani na utulivu nchini.
Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Afrika na imeridhia Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (African Charter on Human and Peoples Rights). Kwa kuridhia mkataba huo, Tanzania inapaswa kutekeleza Haki za Binadamu kama zilivyoainishwa katika Mkataba huo pamoja na miongozo mingine ya Haki za Binadamu ambayo imebuniwa kwa mujibu wa Mkataba huo.
ACHPR imepewa mamlaka ya kusimamia haki za binadamu barani Afrika kama zilivyoainishwa katika Mkataba.
Ili kufanikisha majukumu yake, ACHPR imekuwa ikishirikiana na Taasisi za Kitaifa za Haki za Binadamu kama vile Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa upande wa Tanzania. THBUB ina hadhi ya mwanachama shirikishi (affiliate member) katika ACHPR.
THBUB inatoa wito kwa wadau kuonesha ushirikiano ili tuwe na mifumo mizuri itakayoimarisha haki za binadamu nchini Tanzania.
Pamoja tunaweza, tekeleza wajibu wako, tulete maboresho katika mfumo wa haki-jinai nchini.
Asanteni kwa kunisikiliza.