Tanzania Kunufaika Zaidi na Bandari ya Mtwara na Tanga

Rais wa Chama cha Wakala wa Forodha na Uondoshaji wa Shehena Tanzania (TAFFA) Bw. Stephen Ngatunga akisisitiza kuhusu serikali kulifanyia kazi suala uundaji wa mkakati wa kutangaza bandari zetu nje ya nchi kwa kufungua ofisi katika nchi zinazotuzunguka kwa lengo la kuongeza watumiaji wa bandari . Kushoto ni Mkurugenzi mshauri wa TAFFA na Bw. Jimmy Mwalugerwa (Mkurugenzi TAFFA).

Na Aron Msigwa – MAELEZO, Dar es Salaam
 
IMEELEZWA kuwa Tanzania itanufaika zaidi kibiashara kupitia bandari ya Dar es salaam, Mtwara na Tanga kutokana na serikali kuamua kufanya maboresho  makubwa katika sekta ya usafiri wa Bandari na reli.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es salaam na Rais wa Chama cha Wakala wa Forodha na Uondoshaji wa Shehena Tanzania (TAFFA) Bw. Stephen Ngatunga wakati akitoa ufafanuzi kuhusu mkutano wa Kimataifa wa Wakala wa Forodha katika nchi za Afrika na Mashariki ya kati (RAME 2013) utakaofanyika jijini Dar es salaam kuanzia Juni 19.

Amesema Tanzania kupitia Chama cha Wakala wa Forodha na Uondoshaji Shehena Tanzania (TAFFA) itakuwa mwenyeji wa mkutano huo utakaowashirikisha mawakala 300 wa makampuni ya usafirishaji na upokeaji wa mizigo, wafanyabiashara, maafisa wa serikali na mabalozi mbalimbali kutoka nchi za Mashariki ya kati.

Amesema mkutano huo wa siku 3 utakuwa na manufaa makubwa kwa wafanyabishara kutoka Tanzania kujenga mahusiano na kunufaika na fursa mbalimbali zilizo katika eneo zima la Afrika na Mashariki ya kati, kuitangaza Bandari ya Dar es salaam, Tanga na Mtwara pamoja na kukuza utalii nchini.

Amefafanua kuwa Tanzania kupitia TAFFA  inakuwa mwenyeji wa mkutano huo kutokana na pendekezo lililopitishwa katika  mkutano mkuu wa dunia wa mwaka 2012 uliofanyika mjini Los Angeles, Marekani.

Ameongeza kuwa katika mkutano huo wa Juni 19, rais wa Shirikisho la Kimataifa la Wakala wa Forodha na Uondoshaji wa Shehena (FIATA) Bw. Stanley Lim pamoja na wajumbe waandamizi wa shirikisho hilo kutoka nchi wanazoziwakilisha watajadili mambo mbalimbali ya kuboresha biashara katika ukanda wa nchi za Afrika na Mashariki ya Kati (RAME).

Katika hatua nyingine Bw. Ngatunga amefafanua kuwa  maboresho yanayoendelea hususan katika bandari ya Dar es salaam yanaifanya Tanzania kuwa katika nafasi nzuri ya kupanua wigo wa kunufaika na ongezeko la fursa za biashara kwa nchi zisizo na ukanda wa bahari zikiwemo Burundi, Rwanda , Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Zambia na Malawi kuendelea kutumia usafiri wa reli na Bandari za Tanzania kusafirisha mizigo.

Amesema kitendo cha serikali kufanya maboresho makubwa ya kiutendaji katika bandari na reli  kimesaidia kuendelea kuleta imani kwa wafanyabishara kutoka nchi mbalimbali zisizo za ukanda wa Bahari kupitisha mizigo yao na kuongeza kuwa matatizo mbalimbali yaliyokuwa yakikwamisha uondoshaji wa shehena bandarini yamefanyiwa kazi.

Ameeleza kuwa serikali kukubali kulifanyia kazi suala la ukusanyaji wa mapato ya Bandari na kuagiza lifanyike kupitia benki badala ya utaratibu wa awali wa kulipa fedha moja kwa moja bandarini limepunguza urasimu na kuongeza uwajibikaji na ukusanyaji wa mapato katika sekta hiyo.

“Kwanza suala la ukusanyaji wa mapato bandarini lilisababisha usumbufu mkubwa, waziri wa uchukuzi alivyoingia tulimweleza na tukamwomba alifanyie kazi na jambo hilo likatekelezwa sambamba na uboreshaji wa huduma za usafiri wa reli ili kupunguza mrundikano wa makontena bandarini kanma ilivyoainishwa katika bajeti ya uchukuzi ya 2013/2014 limetufariji sana” ameeleza Bw. Ngatunga.

Aidha ameiomba serikali kulifanyia kazi suala uundaji wa mkakati wa kutangaza bandari zetu nje ya nchi kwa kufungua ofisi katika nchi zinazotuzunguka kwa lengo la kuongeza watumiaji wa bandari na kukabiliana na ushindani pamoja na kuwachulia hatua za kisheria wale wote watakaokwamisha ufanisi wa shughuli za bandari nchini.