Tanzania Kufutiwa Deni la Dola Milioni 220 na Japan

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amewasili nchini Japan leo, Jumatano, Mei 29, 2013, kuhudhuria Mkutano wa Tano wa Kuzungumzia Maendeleo ya Afrika ujulikanao kama Tokyo International Conference on African Development (TICAD – V) unaoanza Yokohama, mji mkubwa wa pili katika Japan, Jumamosi, Juni Mosi hadi 3, mwaka huu, 2013.

Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Narita mjini Tokyo, Rais Kikwete ambaye anafuatana na Mama Salma Kikwete amepokewa na Balozi wa Tanzania katika Japan Mama Salome Sijaona na maofisa wengine wa Ubalozi wa Tanzania katika Japan.

Rais Kikwete amewahi kuwasili nchini Japan kabla ya Mkutano wa TICAD V kwa vile ni mmoja wa viongozi wawili wa Afrika waliopangwa kuonana na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe kabla ya kuanza kwa Mkutano wenyewe wa TICAD V.

Abe ambaye ndiye amemwalika Rais Kikwete kufanya ziara ya kikazi ya wiki moja katika Japan wakati huu anakutana na Rais Kikwete mapema ili kuweza kupata maoni, msimamo na matarajio ya Afrika kabla ya kuanza kwa Mkutano wa TICAD V.

Mkutano wa mwaka huu utakwenda sambamba na sherehe za kumbukumbu ya miaka 20 ya Mkutano wa TICAD ambao ulifanyika kwa mara ya kwanza mjini Tokyo mwaka 1993.

Mkutano huo – TICAD V utawashirikisha viongozi wa Afrika, viongozi wa Japan na washirika wa maendeleo ya Afrika ikiwamo Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) na Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) na utafunguliwa na Waziri Mkuu wa Japan mwenyewe, Mheshimiwa Abe.

Wengine waliopangwa kuzungumza kwenye sherehe hiyo ya ufunguzi wa Mkutano huo mkubwa ni Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika (AU), Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki Moon na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika Mheshimiwa Dkt. Nkosazana Dlamini Zuma.

Mbali na kukutana kwa mazungumzo na Waziri Mkuu Abe, Rais Kikwete pia atakuwa miongoni mwa kundi la viongozi wa Afrika watakaokutana na Mfalme wa Japan, H.M. Akihito.

Katika mkutano kati ya viongozi hao wawili, Waziri Mkuu wa Japan anatarajiwa kuwa atatangaza kuwa Japan inaifutia Tanzania deni la dola za Marekani milioni 220 likiwa ni deni la mchele ambao Tanzania iliupata kutoka Japan chini ya mikataba iliyotiwa saini kati ya mwaka 1980 na 1983 kati ya Mamlaka ya Chakula ya Japan na Serikali ya Tanzania.

Aidha, inatarajiwa kuwa Mheshimiwa Abe atatangaza rasmi kuwa Japan itagharimia ujenzi wa barabara ya juu kwa juu (fly-over) katika eneo la Ubungo, Dar es Salaam, kama moja ya hatua za kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo.

Kabla ya kuanza TICAD V, Rais Kikwete pia atakutana na kuzungumza na wakuu wa mashirika makubwa na kimataifa ya kibiashara na uchumi ya Japan ambayo yanaendesha shughuli zake katika Afrika ama yanapenda kuanzisha shughuli katika Tanzania.

Kesho, Alhamisi, baada ya kuwa amekutana na Mheshimiwa Abe, Rais Kikwete atakwenda Kawasaki ambako atakutana na viongozi wa Kampuni ya Natori Holding Management ambayo imeamua kuwekeza katika sekta ya nguo na kilimo cha pamba katika Tanzania.

Baadaye kesho, Rais atatembea Jumba la Makumbusho la Sayansi la Kampuni ya Toshiba, maarufu duniani kwa utengenezaji wa kompyuta za aina ya Toshiba na vifaa vingine vya elektroniki. Baadaye, Rais atatembelea na kuzungumza na wanafunzi wa Shule ya WASEDA kuhusu nafasi na mchango wa Tanzania katika uhusiano wake na Japan.

Keshokutwa, Ijumaa, Rais Kikwete atatembelea Shirika la Sumitomo ambalo limewekeza katika ujenzi wa kituo cha umeme cha Kinyerezi cha Dar Es Salaam ambacho kitatoa megawati 220 na linataka kuwekeza katika miradi ya miundombinu kwa kushirikiana na sekta binafsi katika Tanzania.

Akiwa Sumitomo, Rais Kikwete atashuhudia utiaji saini wa ujenzi wa mradi wa umeme wa Kinyerezi baina ya Sumitomo Corporation yenyewe, Benki ya Maendeleo ya Japan – JBIC na Wizara ya Fedha ya Tanzania.

Mchana wa keshokutwa, Rais Kikwete atakuwa miongoni mwa viongozi wachache wa Afrika walioalikwa na Waziri Mkuu Mheshimiwa Abe kuzungumzia hali ya Somalia.

Katika mkutano huo, Abe anataka kupata mawazo ya viongozi hao wachache wa Afrika ambayo yatawasilishwa kwenye Mkutano wa 39 wa wakuu wa Nchi Tajiri na Zenye Viwanda Vingi Duniani – G-8 uliopangwa kufanyika Lough Erne, Uingereza mwezi ujao, Juni 17-18, 2013.

Aidha, Rais Kikwete siku hiyo hiyo, atakutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Kampuni ya Marubeni, moja ya makampuni makubwa zaidi ya biashara katika Japan ambayo imeonyesha nia ya kujenga Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia na Kuzalisha Umeme katika Tanzania.

Jioni ya siku hiyo, Rais Kikwete atahudhuria hafla maalum ya kitaifa inayoandaliwa na Mheshimiwa Abe kwa ajili ya viongozi wote watakaohudhuria Mkutano wa TICAD V.

Mkutano wa TICAD V miongoni mwa mambo mengine utajadili mchango wa sekta binafsi, biashara na uwekezaji kama injini za maendeleo, jinsi gani Afrika inavyoweza kuimarisha sekta ambazo zimejithibitisha kuwa misingi ya kukua kwa uchumi wa Bara la Afrika, Ajenda ya Maendeleo baada ya mwaka 2015 ambao ni mwisho wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG’s). Hatimaye, mkutano huo utatoa Azimio ya Yokohama 2013 na Mpango wa Utekelezaji wa Yokohama kwa miaka 2013 hadi 2017.

Mikutano ya TICAD (TICAD Policy Forum and Conference) ilianzishwa mwaka 1993 na Japan kwa kushirikiana na UN, UNDP na Benki ya Dunia kwa njia ya kujadili na kuendeleza ajenda ya maendeleo ya Bara la Afrika.

Chini ya mchakato huo wa TICAD, Japan hujenga mazingira ya kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya Bara la Afrika ambalo nalo ndilo linamiliki na kuongoza jukumu la kimsingi la kujiendeleza kwa kushirikiana na Bara la Asia na Jumuia ya Kimataifa.

Tokea ulipofanyika mkutano wa kwanza – TICAD 1 mjini Tokyo Oktoba 5-6, mwaka 1993, imefanyika mikutano mingine mitatu na kujenga mazingira mazuri zaidi ya jinsi Japan na Jumuia ya Kimataifa inavyoweza kuchangia maendeleo ya Afrika.