Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akikata utepe kuzindua rasmi huduma mpya ya Mfumo wa Utambuzi wa Bidhaa Tanzania, (Global Standard 1 ), wakati wa uzinduzi huo uliofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Julai 04, 2011. Picha na Muhidin Sufiani-OMR
Na Joachim Mushi
MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Dk. Gharib Bilal amesema wafanyabiashara nchini watarajie kunufaika zaidi baada ya Tanzania kuanza kutumika nembo ya mstari inayotumika kwenye kompyuta kutambua taarifa za bidhaa kimataifa (GS1).
Dk. Bilal alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akifungua rasmi nembo hiyo kwenye Maonesho ya 35 ya Biashara Kimataifa katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Saba Saba, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Alisema mfumo huo ni mzuri na utafanikisha kuingiza bidhaa nyingi za Tanzania soko la kimataifa hivyo, wafanyabiashara na nchi kwa ujumla kunufaika kimapato. Alisema mfumo huo unafuatilia taarifa za bidhaa tangu ikiwa shambani hadi inapomfikia mlaji wa mwisho, jambo ambalo linaongeza uthamani wa bidhaa.
Alisema awali wafanyabiashara kutoka nchini walikuwa wakilazimika kununua huduma za nembo hiyo kutoka Kenya, Afrika Kusini na mataifa mengine hivyo kupata usumbufu na gharama kubwa, huku wengine wakishindwa kupata huduma hiyo.
Aliongeza kuwa awali kukosekana kwa huduma hiyo kulizikosesha bidhaa za Tanzania kupata soko zuri kimataifa, kwani zilishindwa kupata ushindani kama lilivyo bidhaa nyingine kwa kukosa taarifa muhimu za bidhaa husika.
“Kama mnavyofahamu hii ni mifumo ya masoko ya kimataifa kuhusu usalama wa chakula unaozingatia mfumo wa ufuatiliaji kutoka shambani hadi mezani, kwa kuweka kumbukumbu sahihi katika hatua zote za mlolongo wa soko. Hatuna budi kuitekeleza mifumo hii ili tuwezeshe bidhaa zetu kuuzika katika masoko ya ndani hususan ‘supermarkets’ na masoko ya kimataifa na kikanda….,” alisema Dk. Bilal.
Alisema GS1 inaumuhimu mkubwa kwani inarahisisha taarifa nyingi za kuwezesha kutambua bidhaa, nchi ilikozalishwa, mfumo wa uzalishaji, ubora na usalama wa bidhaa na ufuatiliaji wa bidhaa yenyewe; jambo ambalo linawavutia wanunuzi kutokana na kuwa na uhakika wa usalama wa bidhaa husika.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Viwanda na Bishara, Dk. Cyril Chami alisema tayari kuna kampuni takriban 120 zimepatiwa elimu ya mafunzo ya mfumo wa ufuatiliaji na mfumo wa kimataifa wa utambuzi wa GS1 ambao ni nyenzo muhimu katika mfumo huo.
Alisema Wizara ya Viwanda na Biashara itahakikisha inatoa ushirikiano wote ili kuweza kufanikisha mfumo huo kuweza kufanya kazi kama inavyotakiwa, kwani mfumo unaoandaliwa utakuwa na manufaa kwa watanyabiashara pamoja na taifa zima kwa jumla.
Kuanzishwa kwa mchakato wa mfumo huo nchini, utawezesha bidhaa za Tanzania nazo kuweza kuuzwa kwa wingi kwenye maduka makubwa ya bidhaa kama supermarkets ambapo awali ilikuwa ni nadra kuonekana kwa wingi.