Tanzania isikubali misaada yenye masharti magumu-Wanaharakati

Mwanaharakati kutoka nchini Ghana, Profesa Dzodzi Tsikata akitembelea mabanda ya asasi anuai baada ya kuzindua rasmi Tamasha la Kumu la TGNP, anayefuatana naye ni Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Malya.

Na Joyce Ngowi

MWANAHARAKATI wa Kimataifa kutoka nchini Ghana, Profesa
Dzodzi Tsikata ameishauri Serikali ya Tanzania kuacha utegemezi wa misaada midogo yenye masharti magumu na badala yake kuangalia namna nzuri ya kutatua matatizo ya raia wake kwa manufaa ya Taifa zima.

Prof. Tsikata ametoa changamoto hiyo leo jijini Dar es Salaam kwenye viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) alipokuwa akitoa mada na kuzindua rasmi Tamasha la Kumi la TGNP).

Aidha mwanaharakati huyo kutoka nchini Ghana amesema tangu kuanzishwa kwa utandawazi waathirika wengi wamekuwa ni wanawake na watoto hasa wale wa vijijini pia wale wapembezoni kwani hawana uwezo wa kifedha wala uamuzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya (kulia) akizungumza leo kwenye Tamasha la Kumi la Jinsia linalofanyika kwenye viwanja vya TGNP jijini Dar es Salaam (Picha zote na Joachim Mushi)


Ameema sera tunazopokea kutoka nchi tajiri zimekuwa zikieleza kuwa sekta binafsi ndiyo zenye kuleta maendeleo jambo ambalo si kweli, kwani mashamba makubwa na taasisi zinazomilikiwa na Serikali zinapo binafsishwa wananchi wamekuwa wakikosa ajira hivyo kuchangia ongezeko la umasikini.

“Tunaishi kwenye nyakati zenye changamoto nyingi ikiwemo tishio
kubwa la njaa na ukame kutokana na kutokuwepo kwa siasa na sera
madhubuti za chakula hii ni pamoja na haki ya kumiliki ardhi
kuonekana ni haki ya watu wachache wenye uwezo,” alisema.

Hata hivyo amefafanua kuwa baadhi ya wawekezaji kutoka nje ya nchi
wanazifanya nchi kuwa maskini kwa kutothamini michango ya wenyeji
wa maeneo wanayokwenda kuwekeza hivyo wananchi wasikubali mikataba
ambayo imekuwa haiwashirikishi.

“Changamoto nyingi zinazojitokeza katika suala la umikaji wa ardhi
zinatokana na sheria zilizotumika na waathirika wakubwa ni wanawake na watoto hivyo kuna haja ya kushirikiana ili kutatua tatizo hili,” alisema.

Amesema umefika wakati nchi za Afrika Mashariki zikaangalia
upya suala la wawekezaji kwa kufahamu athari na faida kabla ya
mwekezaji kupewa ardhi. Profesa Tsikata alisema kutokana na ukosefu wa ardhi vijana wengi hujikuta wakikosa ajira huku wanawake wakidanganywa kwa kupewa mikopo midogo midogo isiyokuwa na faida.

“Hii mikopo midogo midogo tunayopewa na isiyokuwa na faida sasa imefika wakati tusikubaliane nayo kwani tukiiendekeza inarudisha nyuma maendeleo hasa muhusika anaposhindwa kurejesha deni na kubebewa kile alichonacho hata kama ni kidogo,” alisema.

Akifungua tamasha hilo lililokuwa na msisitizo unaoeleza”Jinsia Demokrasi na maendeleo mkurugenzi wa TGNP, Usu Mallya alisema tamasha hilo limehudhuriwa na zaidi ya watu 2500 kutoka katika nchi mbalimbali ikiwemo Marekani, Ghana, Zambia, Rwanda, Burundi, Kenya na wawakilishi toka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.

Mkurugenzi huyo alisema tamasha hilo limeandaliwa kwa kushirikiana
na Femac, UN, DANIDA, SIDA pamoja na mashirika mengine, hivyo kuwataka washiriki kutambua ni wapi tunatoka na wapi tunaelekea kwa kipindi cha tangu miaka 50 ya Uhuru.

Baadhi ya wanaharakati na wageni waalikwa mbalimbali kutoka nje ya nchi wakishiriki katika Tamasha la Kumu la Jinsia, linaloendelea jijini Dar es Salaam.