Tanzania Ina Vikwazo vya Kibiashara – Dk Nagu
Na Gervas Yohane, Rombo
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mery Nagu, amesema Tanzania ni moja kati ya nchi ambayo ina gharama kubwa katika kufanya biashara, hali inayochangia wawekezaji kutofikiria kuwekeza nchini.
Dk. Nagu aliyasema hayo jana wakati alipotembelea jengo la kutoa huduma kwa pamoja, (one stop border), lililojengwa eneo la Holili Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro. Waziri Nagu alisema Tanzania ina garama kubwa za kufanya biashara, na kwamba gharama inapokuwa kubwa madhara yake wawekezaji hawawezi kuja kuwekeza hivyo nchi inashindwa kuwa na ushindani.
“Sisi hatutakuwa na nguvu ya ushindani katika nchi zingine kwa sababu ya nchi hii kuwa na garama kubwa katika kufanya biashara ndio maana tuko nyuma kimaendeleo,” alisema Nagu.
Hata hivyo waziri huyo alipongeza ujenzi wa kituo cha Holili na kudai hatua kilipofikia kinatia matumaini kwani vituo vingi vya mipakani upande wa Tanzania vilikuwa katika hali mbaya.
“Kuwepo wa kituo hicho kitasaidia kupunguza gharama hivyo kuwavutia wafanyabiashara wengi zaidi kuja kuwekeza hapa nchini,” alisema Nagu.
Aidha alisema kuwa vituo vya namna hiyo vitasaidia kutarahisisha kazi na kupunguza muda wa wafanyabiashara kuingiza na kusafirisha mizigo kwa urahisi hivyo kuchangia ufanisi katika biashara. Naye kaimu mkuu wa kituo cha forodha Holili, Nassor Salim Juma, alisema kuwa kukamilika kwa kituo hicho kunakotarjiwa kufanya hivi karibuni na kwamba kinatarajiwa kutumika kama kilivyokusudiwa.