Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Tanzania imeeleza utayari wake wa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jumuiya ya Afrika Mashairiki ili kuifanya jumuiya hiyo iwe na mafanikio na itaendelea kushirikiana na nchi nyingine wanachama kutatua changamoto zinazojitokeza.
Hayo yalielezwa jijini Dar es Salaam wiki hii na Makamu wa Rais wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal alipokutana na jopo la wataalamu kutoka Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM)
Dk. Bilal akijibu swali la jinsi gani Tanzania inashiriki katika
jumuiya hiyo kama Jamhuri ya Muungano, aliwaeleza wataalamu hao kutoka nchi zaidi ya 20 za Afrika kuwa pamoja na Tanzania kuwa ni Muungano wa nchi mbili ushiriki wake katika EAC ni wa pamoja.
“Tunawashirikisha wenzetu wa Zanzibar na kwa hiyo tunashiriki kama
nchi moja. Hata kama kuna changmoto za hapa na pale lakini Tanzania
inabaki kuwa mwanachama mwaminifu wa EAC,” alisema Dk. Bilal katika
mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zaidi ya 30 za Afrika zilizojiunga na
mchakato wa APRM na tayari imekwishajifanyia tathmini ya ndani kuhusu utawala bora na ripoti ya nchi inapitiwa upya kwa sasa na wataalamu hao wanaoongozwa na Wakili Akere Muna kutoka Cameroun.
Ujio wa wataalamu kutoka nchi nyingine za Afrika ni hatua muhimu
katika hatimaye kuifanya nchi inayoshiriki mchakato wa APRM, kuanza
kutekeleza Mpangokazi wa Kitaifa wa kushughulikia uondoaji wa kero za
kiutawala bora zilizobainishwa katika ripoti.
Akizungumza wakati wa kuzindua uhakiki huo Machi 7 mwaka huu, Rais
Jakaya Kikwete alisema kuwa Tanzania iko tayari kutekeleza mapendekezo yatakayotolewa na wataalamu hao ili kuboresha utawala bora nchini.
Wakati huo huo, mchakato wa APRM umeelezwa kuwa ukombozi kwa wananchi wan chi za Afrika kuweza kueleza hisia zao kwa Serikali ili kuleta maendeleo ya pamoja.
Ufafanuzi huo umetolewa na Prof. Ahmed Muhiddin kutoka Kenya ambaye ni mmoja wa wataalamu waliopo nchini kutoka APRM makao makuu alipokuwa akifafanua juu ya faida za mchakato huo wakati wa kikao kati ya wataalamu hao na wawakilishi wa mashirika ya wabia wa maendeleo wanaohusika na utawala bora, Dar es Salaam jana.
“Uzoefu kutoka nchi mbalimbali za Afrika zinazoshiriki mchakato huu
unaonesha kuwa APRM imekuwa daraja kati ya wananchi na Serikali zao. Kupitia APRM wananchi sasa wanaweza kuishauri Serikali na Serikali
ikawasikiliza,” alisema Prof. Muhiddin.