Tanzania Hatiani kwa Kukiuka Haki za Binadamu…!

Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli

Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli

Na Baltazar Nduwayezu, EANA

MAHAKAMA ya Afrika kuhusu Haki za Binadamu na za watu (AfCHPR) imeitia hatiani serikali ya Tanzania kwa kukiuka haki za binadamu katika kesi dhidi ya raia wakenya wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji na ujambazi wa kutumia silaha.

Raia hao kumi wa Kenya waliwasilisha shauri lao Mahakama ya Afrika mwaka 2013, wakilalalmikia ukiukwaji wa haki za binadamu katika kukamatwa kwao na katika mwenendo mzima wa kesi yao. Walilalamikia kesi yao kuchukua muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuahirishwa mara 55 ndani ya miaka kumi tangu kukamatwa kwao kwa kisingizio cha kukamilisha upelelezi, halikadhalika kesi yao kusikilizwa bila wao kuwa na mawakili wa kuwatetea.

Akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya majaji wenzake tisa kati ya 11 wa Mahakama ya Afrika, Jaji Fatsah Ouguergouz kutoka Algeria amesema kuwa Mahakama imeamuru serikali ya Tanzania kuwapa walalamikaji mawakili wa kuwatetea katika kesi yao ambayo kwa sasa iko kwenye ngazi ya rufaa. Rais wa Mahakama hiyo, Augustino Ramadhani, Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, hakushirkia katika kesi hiyo, kwa maelezo kwamba kesi ilihusu serikali ya nchi yake.

“Mahakama inaamuru pia Mshtakiwa (serikali ya Tanzania) kuchukua hatua za makusudi za kuharakisha na kumaliza rufaa zote dhidi ya mlalalmikaji katika mahakama za nchi” aliendelea kusoma Jaji Fatsah na kujulisha Mahakami hii ni hatua gani zimechukuliwa ndani ya miezi sita baada ya hukumu hii”.

Mahakama imeagiza walalamikaji kuwasilisha ndani ya siku 30, mapendekezo ya fidia juu ya uonevu waliofanyiwa, huku serikali ikipewa muda wa siku thelathini baada ya kuwasilishwa hayo mapendekezo, kutoa maoni yake.

Wakifafanua uamuzi wao katika hukumu hiyo, majaji walisisitiza kuwa mtu anavyokamatwa ni wajibu wa majaji kuchukua hatua stahiki ili kuendesha kesi kwa haraka, na kuwajibisha pande zote zinazohusika kwenye kesi (upande wa mashtaka na upande wa utetezi) pale zinapoelekea kukwamisha kesi.

Halikhadhalika ni wajibu wa majaji kuhakikisha kwamba washtakiwa wanapewa utetezi hata kama hawajauomba, ili kesi iwe ya haki. Mahakama imetupilia mbali hoja zote za serikali ya Tanzania ilizowakilisha kupinga Mahakama hii kupokea shauri hili.

Suala la madai ya wakenya hao kutekwa na kuletwa Tanzania kwa nguvu wakitolewa Msumbiji halikujadiliwa na Mahakama kwa misingi kwamba haliko kwenye mamlaka waliyo nayo. Mawakili wa utetezi ambao ni Chama Cha Wanasheria wa Afrika (PALU) hakikufurahishwa na jambo hilo.

“Tumefurahia uamuzi wa mahakama leo kwa kuwatendea haki wateja wetu, ila hatujaridhika na hatua ya Mahakama ya kutojadili suala la kutekwa wateja wetu wakati wanakamatwa, maana nao ni ukikukwaji wa haki za binadamu, maana ukamataji wahalifu nao una sheria zake. Labda litakuwa jambo la busara wahusika kuangalia namna ya kurekebisha Mkataba wa Afrika kuhsu haki za binadamu na za watu, na kuingiza suala la utekaji” alisema baada ya hukumu kutolewa, Bi Evelyn Chijarira, mshauri wa masuala ya sheri kwenye PALU.

Naye Mwakilishi wa Tanzania Mwanasheri mwandamizi Mark Mulwambo amesema kuwa Mwanasheri mkuu wa serikali atatoa kauli ya serikali juu ya hukumu hiyo baada ya kupitia kwa kina hukumu kama alivyoandikwa. Raia hao wa Kenya waliowasilisha kesi Mahakama ya Afrika ni Wilfred Onyango Nganyi, Peter Gikuru Mburu, Jimmy Maina Njoroge, na Patrick Mutheee Muriithi.

Wengine ni Simon Githinji Kariuki, Boniface Mwangi Mburu, David Ngigu Mburu, Gabriel Kungu Kariuki na Simon Ndungu Kiambuthi. Wenzao wawili walifariki dunia wakiwa katika magereza ya Tanzania, ambao ni Peter Kariba na John Odongo Odhiambo.

Wakenya hao walikamatwa miaka kumi iliyopita mjini Maputo nchini Msumbiji, na kuletwa Tanzania kwa ndege ya jeshi, na baadaye kuhukumia kufungwa miaka 30 jela, baada ya kukutwa na hatia ya kosa la mauaji na ujambazi wa kutumia silaha lililofanyika katika benki ya NMB Tawi la Moshi, mwezi Mai, 2004.