Na Mwandishi Wetu
Namanga
LICHA ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) kutakiwa kulipa deni la sh. bilioni 94 kwa kampuni ya Dowans ambazo bado zimeleta utata, imebainika kuwa shirika hilo pia linadaiwa sh. milioni 175 na Shirika la Umeme nchini Kenya (KPLC).
Shirika hilo la kusambaza umeme Kenya, limekuwa likitoa huduma ya umeme katika baadhi ya maeneo yaliyo mpakani mwa nchi hiyo na Tanzania, ikiwemo Namanga upande wa Tanzania na Longido mkoani Manyara.
Akifafanua juu ya deni hilo jana, Meneja Mkuu wa KPLC, Josh Orodo, alisema kuwa deni hilo ni la utoaji wa huduma za umeme wa takribani miaka miwili unaofanywa na kampuni yake sehemu hizo za Tanzania.
Alisema japokuwa deni hilo halijalipwa na TANESCO bado kampuni hiyo kutoka Kenya inaendelea kutoa megawati 0.2 za umeme ambao unasambazwa nchini katika baadhi ya maeneo, hali ambayo inaongeza ukubwa wa deni.
Jambo Leo lilipomtafuta Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, William Mhando kuzungumzia madai hayo, alikanusha vikali na kusema kuwa KPLC haiwadai fedha.
Alisema kuwa kulingana na masharti ya mkataba, iwapo TANESCO ingekuwa inadaiwa umeme huo ungelikuwa umekatwa, na kwamba anashangaa kusikia deni hilo wakati umeme ukiendelea kuwaka.
“Sisi hatudaiwi chochote na KPLC, ukitembelea maeneo hayo unaweza ukaona umeme ukiwaka, sasa kama wanadai kwanini wasisitishe huduma ya umeme kama ambavyo mkataba unataka?” alisema Mhando.
Hata hivyo, watati Orodo alipokuwa akizungumza kuhusiana na deni hilo, alikuwapo Mkuu wa kituo cha TANESCO eneo hilo la Namanga, Leo Mrisha, ambaye alikiri kuwapo kwa deni hilo na kwamba madai alikwisha yawasilisha Makao Makuu.
Aliongeza kuwa KPCL imekuwa ikiendelea kutoa huduma kutoka na uungwana, ingawa bado inawadai. Aidha Orodo alisema kuwa Kenya inazalisha umeme wa majenereta makubwa yatumiayo mafuta ya diseli na ndio tegemeo la nishati hiyo muhimu kwa Taifa.
Aliongeza kuwa uzalishaji wa umeme kwa kutumia majenereta ni wa gharama, hasa ikizingatiwa bei ya mafuta hayo ni ya juu huku ilhali maitaji yanazidi kuongezeka.
Orodo alisema Kenya imefanikiwa kiasi kikubwa katika uzalishaji wa nishati hiyo na hadi sasa asilimia 80 ya wananchi wanapata nishati ya umeme kwa matumizi mbalimbali.
Alisema asilimia iliyobaki wananchi hawawezi kulipia gharama za umeme na Serikali inafanya utaratibu wa kuwasaidia. Lengo ni kufikia asilimia 100.