TANAPA yatakiwa kuilipa TBC mil 52.2/-

 

 

Mwenyekiti wa Kamatai ya Bunge ya Hesabu ya Mashirika ya Umma, Mh. Zitto Kabwe (Mb)

Benjamin Sawe – Maelezo
Dar es Salaam
KAMATI ya Bunge ya Hesabu ya Mashirika ya Umma imeliagiza Shirika la Taifa la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kulipa deni la sh. milioni 52.2 linalodaiwa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ikiwa ni deni la matangazo ya shughuli za shirika hilo.

Uamuzi huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zito Kabwe wakati kamati yake ilipokutana na baadhi ya viongozi wa TANAPA katika Ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam jana.

Kabwe alisema katika barua ya TANAPA iliyoandikwa Agosti 11, mwaka 2010 iliyoandikwa kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC walikiri kuwa walipata huduma hiyo ya matangazo kupitia shirika hilo na kwamba deni wanaladaiwa ni la halali.

 
Mwenyekiti huyo aliwaambia viongozi wa TANAPA kuwa kwa kuwa katika barua yao walikiri kuwa deni wanalodaiwa ni la halali hivyo aliwataka walilipe kwa muda wa siku ya leo (jana) na kesho (kesho kutwa). Aliongeza kuwa mara watakapolipa deni hilo wanapaswa kuiandikia barua kamati hiyo kuwa wameshalilipa deni hilo.

Aidha Zito alisema kamati yakeilipokutana na baadhi ya viongozi wa TANAPA, Machi mwaka huu iliwapa lengo la kukusanya sh. bilioni 150 na kusema kuwa hana tatizo na ukusanyaji huo wa mapato ya shirika hilo.

 
Alisema toka kipindi hicho TANAPA mpaka sasa hivi wameweza kukusanya mapato ya Shs bilioni 105 hivyo hawawezi kulipima lengo hilo kwa kuwa ni kipindi kifupi tangu wakubaliane hivyo utekelezaji utaangaliwa katika mahesabu yanayoishia Juni 2011.

Wakati huo huo Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Allan Kijazi aliahidi kulilipa deni hilo mapema iwezekanavyo na watatoa taarifa kamili kwa kamati hiyo mapema iwezekanavyo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha malengo yanatimia kama ilivyopangwa.