MKURUGENZI Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Bi. Eda Sanga akizungumza kabla ya ufunguzi wa mafunzo hayo alisema TAMWA ina kila sababu ya kuingia katika mapambano ya ajali nchini kwa kuwa zimekuwa zikiwaathiri wanawake na watoto kwa kiasi kikubwa. Alisema licha ya ajali nyingi kupoteza maisha ya wanaume na kujeruhi wengine kundi hilo limekuwa likiwaacha wake zao na watoto pasipo na msaada kwa kuwa wengi humtegemea baba kama mtafutaji katika familia.
Alisema wanawake wanaoachwa peke yao na familia wamekuwa wakibeba mzigo mkubwa wa familia jambo ambalo limeendelea kuwaingiza katika hali ngumu. Aidha aliongeza kuwa pamoja na hayo ajali nyingi za waendesha pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda zimekuwa zikiwaathiri akina dada na akina mama ambao ndio watumiaji wa vyombo hivyo vya usafiri kiasi kikubwa.
Tamwa katika mradi huo imejikita katika kutoa elimu ya madereva kuepuka ulevi, ufungaji mikanda ya usalama katika magari, mwendo kasi na matumizi ya kofia ngumu kwa waendesha pikipiki pamoja na abiria wao.
Kwa upande wake Mwasilishaji mada kutoka Safe Speed Foundation, Henry Bantu alisema suala la usalama barabarani si jukumu la taasisi moja hivyo kila mtu anapaswa kushiriki katika kupambana na hatimaye kutokomeza ajali hizo ambazo zimekuwa zikipoteza roho za watu, mali pamoja na kusababisha ulemavu kwa baadhi ya waathirika wa ajali hizo.