TAMWA kuwanoa wanahabari 30 kuripoti vitendo vya ukatili

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya.

Na Mwandishi Wetu

WAANDISHI wa habari 30 kesho Ijumaa ya Oktoba 21, 2011 watakutana jijini Dar es Salaam kuimarisha ujuzi wa kutafuta na kuripoti kwa mafanikio vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa vikiwaathiri zaidi wanawake, wasichana na watoto.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake, Ananilea Nkya amesema wanahabari hao watatoka vyombo anuai vya habari nchini.

Amesema ukatili wa kijinsia ni moja ya changamoto kubwa zinazokwamisha juhudi za taifa kuhakikisha kuwa wanawake na wanaume, vijijini na mijini wanafurahia usawa na amani ili waweze kutumia fursa zilizopo kuimarisha maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.

Wanahabari hao watadokezwa jinsi ya kupata taarifa na takwimu za vitendo vya ukatili, wapi pa kupata taarifa hizo, mbinu za kuwahoji waliofikwa na mikasa ya vitendo vya kikatili na jinsi ya kuandika habari za ukatili zinazoweza kushawishi na kuhamasisha hatua kuchukuliwa dhidi ya vitendo hivyo.

Baada ya mafunzo hayo wanahabari hao watatakiwa kujituma kufanya kazi za mfano kulingana na mafunzo hayo na wale watakaofanya kazi nzuri baadaye watapata fursa ya kwenda mikoani kukusanya taarifa na kuandika habari za kiuchunguzi kuhusu ukatili wa kijinsia.

Tafiti zinaonesha kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vilivyoshamiri nchini ni pamoja na kuwaozesha kwa nguvu watoto wa kike ili familia zipate mahari, ubakaji unaosababisha mimba mashuleni na maambukizi vya Virusi vya UKIMWI miongoni mwa wasichana, kurithi wajane nakunyima watoto wa kike na wa kiume haki ya kupata elimu kwa vizingizio mbali mbali.

Ukatili mwingine ni pamoja na kuuwa au kuchuna ngozi walemavu wa ngozi, vipigo na kutoa lugha za matusi kwa kwa wanawake, ukeketaji unaowaweka wanawake katika hatari ya kufa wakati wa kujifungua na kutelekeza watoto kunakochangia wimbi la watoto wa mitaani.

Aidha katika taarifa hiyo, Nkya amesema mafunzo hayo yatakayofanyika katika Ofisi za TAMWA kuanzia saa tatu asubuhi ni sehemu ya kampeni ya kitaifa yenye lengo la kuhamasisha wanannchi, viongozi kuanzia ngazi ya kitongoji hadi taifa, mashirika ya kimataifa ya maendeleo, mashirika ya kijamii ikiwa ni pamoja na taasisi za dini kuchukua hatua kuzuia vitendo vya ukatili na kutoa huduma za afya, msaada wa kisheria na makazi inapolazimu kwa waathirika wa vitendo vya ukatili.

TAMWA imeandaa mafunzo hayo kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya idadi ya watu (UNFPA) kama sehemu ya shughuli za pamoja za Umoja wa Mataifa. Utafiti wa Kitaifa (DHS) wa mwaka 2010 unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 39 ya wanawake hapa nchini wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili tangu wakiwa na umri wa miaka 15 na kwamba wengi wanafanyiwa ukatili na wanaume waume au baba zao ambao ndio wana jukumu kulinda usalama na maslahi ya wanawake, wasichana na watoto.