BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA BARUA YA KICHUNGAJI
“Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu” (Lk. 21: 19)
Sisi Maaskofu wenu tulikutana kusali na kutafakari pamoja huko Arusha tarehe 16 – 17 Februari 2015. Moja ya mambo tuliyoyazingatia ni suala lililo mbele yetu, la kupigia Kura ya Maoni Katiba Inayopendekezwa.
Tunazidi kuendelea kukumbusha kwamba Katiba ni chombo kitakatifu, kinacholenga kufikia maridhiano kama taifa juu ya namna tunavyotaka kuishi pamoja kwa amani na utulivu. Tunapotafakari kipindi chote cha mchakato wa kuunda Katiba, tunaona mazuri mengi yamefanyika. Lakini yapo mambo mengine ambayo yamefanyika na yametugusa na kutufanya tuhofie namna mambo yanavyoweza kujengeka na kuleta madhara katika nchi yetu. Hali hiyo inatulazimu kujiuliza kwa tafakari: Je, tutaweza kuendelea kudumisha amani na utulivu?
1. Mashaka yetu
Hadi sasa Katiba Inayopendekezwa haijawafikia watu wengi.
Hatua muhimu mno ambayo ni kuelimisha watu juu ya Katiba Inayopendekezwa haijafanyika, kwahiyo wananchi wengi hawana ufahamu wa kutosha juu ya maudhui na misingi yake.
Zoezi la uandikishaji wa wapiga kura katika daftari la kudumu la wapigakura halijafikia hatua yenye mwelekeo wa kulikamilisha. Hii inatupa mashakama kubwa sana na hatuwezi kuamini kuwa zoezi hilo litakamilika kabla ya tarehe ya kupiga kura ya maoni.
Katika hali hii tunabaki na mahangaiko na mashaka makubwa ya kutakiwa kupigia Kura Katiba Inayopendekezwa ambayo hawaielewi kikamilifu wala kujua matokeo yake kwa mustakabali wa Taifa letu. Tunajiuliza, katika mazingira kama haya amani haitatetereka? Bahati mbaya sana wanasiasa viongozi wa nchi wanaendelea kutoa maelezo ya kisiasa yanayotoa majibu mepesi kwa maswali magumu, kwa lengo la kufanikisha malengo yao binafsi ya kisiasa. Huu siyo muda wa kufanya hivyo!
Pamoja na mahangaiko na mashaka juu ya suala la Katiba, bado yapo mambo mengi mazito yanayoleta fadhaa kwa jamii yetu:
Mfululizo wa matukio ya mauaji na/au kunyofolewa viungo ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi (Maalbino).
Kuibuka kwa makundi ya wezi na vibaka wakijigamba na kujipachika majina kama panya road, mbwamwitu. Uvamizi wa vituo vya polisi ambapo watu hujeruhiwa wakiwemo askari, na hata kuuawa na silaha kuporwa. Matumizi ya nguvu kupita kiasi yafanywayo na vyombo vya sheria na vyombo vya ulinzi dhidi ya mikusanyiko ya watu.
Hali ya wasiwasi na hofu inayoendelea kujengeka miongoni mwa waumini wa dini mbalimbali, ambayo inaonekana matokeo yake ni kuligawaTaifa. Mifumo ya kutoa haki inakwama mno kutokana na mienendo ya kifisadi inayozidi kuota mizizi.
Taasisi za Serikali zinashindwa kuwapatia wananchi wengi haki zao za msingi.
2. Msimamo wetu juu ya Mpango wa Kura ya Maoni.
Tuangaliapo hali ya nchi yetu leo, tunapata hofu kwamba uharakishwaji wa zoezi hili unaongeza fadhaa na mpasuko ambao tayari upo katika jamii yetu. Watu watawaka hasira kwasababu wanaelewa maoni yao waliyotoa na kuzingatiwa na Rasimu II (ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba) hayakuheshimiwa. Badala yake matakwa ya kisiasa ya watu wachache ndio yamepewa uzito mkubwa katika KatibaInayopendekezwa. Katika muktadha huu msimamo na Ushauri Wetu ni:
Zoezi la kupitisha KatibaInayopendekezwa lipewe muda zaidi/liahirishwe, na kufanyika baada ya Uchaguzi Mkuu, Oktoba 2015.
Tuonavyo sisi, sio jambo la busara kuendelea kuwataka watu kupigia kura kitu wasichokijua. Ikiwa watawala wataendelea kulazimisha, basi wananchi wajitokeze na kupiga kura ya kuikataa Katiba Inayopendekezwa.
Bado tunakumbuka vizuri, jinsi mchakato wa kupata Katiba mpya ulivyoendeshwa kupitia Bunge Maalum la Katiba. Kwa ufupi, uadilifu ulikosekana, dhamiri za wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba ziliingiliwa na wengi wao kulazimishwak utenda kwa hofu na unafiki, uwazi ulikosekana, sheria haikuzingatiwa na roho ya sheria yenyewe haikupewa tafakari stahiki.
Tunabaki kujiuliza motisha wa viongozi wa kisiasa na serikali kulazimisha maoni yao ulitokana na nini? Je, walisukumwa na moyo wa uzalendo ama matakwa ya kibinafsi? Bado tunaamini kuwa walisahau kwa makusudi kwamba suala hilin linadai uwajibikaji mkubwa kwa ajili yaTaifa letu.
Hitimisho
Tunawasihi waumini wetu kuendelea kuombea amani taifa letu na kufanya kila linalowezeka ili kuimarisha na kudumisha amani. Tunaiomba Serikali kutumia mamlaka yake na vyombo vyake vya sheria na vya ulinzi na usalama kujenga amani na kuhimiza ushiriki wa watu wote katika masuala yanayolihusu Taifa letu.
Tunawasihi viongozi wa dini zote na kuwatia moyo watambue kwamba wao ni wadau wa kwanza katika kujenga umoja na moyo wa kupokeana kwa stahamala bila kujali tofauti zetu za kidini. Tunaendelea kukazia UTAKATIFU wa mchakato wa kuunda Katiba ambayo lazima iwe chombo cha kulinda tunu na matakwa/matamanio ya watu wote, na sio ya wachache tu.
Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, name nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta, nakuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote (Yer 29: 12 – 13).
Imetolewa na Maaskofu wa Baraza la Maaskofu Katoliki – Tanzania
+Tarcisius NGALALEKUMTWA
RAIS WA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA