Na Eliphace Marwa – Maelezo
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, George Simbachawene amewaagiza Wakurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa waanzishe zoezi la kubainisha mipaka ya asili ya maeneo yote na kuyapima na kuhakikisha yana hati.
Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Simbachawene amesema kuwa kuna tatizo kubwa la uvamizi wa maeneo ya Shule za Msingi, Sekondari, Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya, hospitali za mikoa na maeneo ya masoko.
“Kwa kuwa uvamizi huu umefanyika katika maeneo mengi nchini hadi kufikia hatua ya kusababisha mwingiliano usiokubalika kati ya huduma zinazopaswa kutolewa na shughuli zinazofanywa na waliovamia maeneo hayo,” alisema Waziri Simbachawene.
Akibainisha aina za uvamizi huo Waziri Simbachawene alitaja kuwa ni ujenzi wa nyumba za makazi ndani ya maeneo hayo, ujenzi wa vyumba vya kufanyia biashara kwa kuzunguka maeneo hayo pamoja na uporaji ardhi iliyotengwa na Serikali kwa matumizi ya ujenzi wa shule, Zahanati na Masoko.
Waziri Simbachawene amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia zoezi hili kikamilifu kwenye malaka za Serikali za Mitaa zilizopo kwenye maeneo yao na zoezi hili litekelezwe ndani ya miezi mitatu. Aidha Waziri Simbachawene amesema kuwa maendelezo yote yaliyofanywa na yanayotarajia kufanywa hayaruhusiwi na kwa shule za msingi na sekondari zilizoko mjini Halmashauri zihakikishe zinajenga uzio kuzunguka shule hizo.
“Wananchi waliovamia maeneo ya taasisi hizo waondoke wao wenyewe vinginevyo hatua za kuwaondoa kwa nguvu zitatumika,” alisema Waziri Simbachawene.
Waziri Simbachawene alitoa wito kwa jamii zinazozunguka maeneo hayo kuhakikisha wanashirikiana na serikali kutoa taarifa kwa mamlaka za serikali za mtaa juu ya uvamizi huo kwa kuonesha alama za asili za mipaka ya maeneo hayo kabla ya kuvamiwa.