TAMASHA la kuhamasisha masumbwi mkoani Mtwara lilimalizika kwa mafanikio mazuri kwa watu kuitikia na kukubali mapambano mengine mengi ya ngumi kufanyika mkoani humo. Katika tamasha hilo lililosindikizwa na pambano la ubingwa wa taifa la uzito wa unyoya kati ya Bakari mohamed’dunda wa blackmamba ya mtwara alimshinda abdala seleman wa Dar es Salaam.
Naye bondia mkongwe Rashid ‘Snake Man” Matumla alimshinda kiaina yake bondia Patrick Amote wa Kenya katika pambano ambalo liliwasisimua mashabiki ambapo idadi kubwa ya mashabiki walionekana kushindwa kukaa vitini muda wote wa pambano na hasa pale Mkenya alipokwenda chini kwa konde zito lililotupwa na Matumla baada ya kukwepa ngumi ya mpinzani wake. Hata hivyo mwanzo alianza taratibu na kuonekana kama mchovu kutokana na kitambi alichonacho na kujikwaakwaa ulingoni lakini kadiri muda ulivyosogea ndivyo alivyobadilika na kuonekana mzuri zaidi.
Pambano jingine lililowavuta tena wapenzi wa Mtwara huku ukimya ukiwa umetawala na mshangao ni la Haruna Mnyalukolo wa Dar na Ashraf wa Blackmamba, kwani ngumi zilipoanza mabondia walianza kwa nguvu kwa kutupiana makonde mfululizo yaliyomuingia kila mmoja na kusababisha kila mmoja kumwangusha mwenzake chini kwa zamu na wote walivimba nyuso na kutokwa na damu baada ya kupasu. Lakini bondia Ashraf uvumilivu ulimshinda raundi ya nne baada ya kukataa kurudi uringoni akiwa mapumziko, pambano hilo lilikuwa la raundi sita.
Wakati huo huo; kocha wa ngumi za kulipwa Christopher Mzazi kutoka katika gym ya “no talking” ya mabibo ya jijini Dar es Salaam ameamua kuwapoza machungu mabondia chipukizi waliopiganishwa na promota Kaike na kutolipwa kwa kuwaandalia pambano litakalopigwa Novemba 18, 2012 Mabibo katika Ukumbi wa D.I.D, pambano litakuwa ni kati ya Mwaite Juma na Baina Mazola. Ni pambano la kiupinzani kwani wawili hao walikuwa wanatafutana baada ya kunusurika kuzipiga kavu kavu.
Akilizungumzia pambano hilo kocha Mzazi alisema ‘Issa Omar na Mwaite Juma ni mabondia wanaofundishwa na kocha mzuri mwenye uwezo mkubwa pia ni mabondia wazuri na ni tegemeo zuri la baadae, sijui kwanini kaike kaamua kuwafanyia uhuni wa kuwadhulumu, hivyo mimi nikiwa kama mzazi kama jina langu nikaona ni vema nikawapoza machungu kwa kuwapa pambano na mabondia wangu na kuwalipa zaidi ya pesa walizodhulumiwa kwa kuwa ninaelewa machungu na ugumu wa mchezo wenyewe ulivyo.
Hivyo basi Mwaite Juma kutoka BigRight boxing gym atacheza na Baina Mazola wa No talking gym katika pambano la raundi nane. yakisindikizwa na karim Ramadhan (mdogo wake nasibu Ramadhani-bondia bora wa mwaka) atakaecheza na martin Richard. Siku hiyo pia kutakuwa na mapambano mengi ya kiushindani ya kuwekana sawa nani zaidi ya mwingine kati ya mabondia wa mabibo na Mwananyamala.