Tamasha La Jinsia 2011 Laja!

 

 

Na Edson Kamukara

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na mtandao wa mashirika watetezi wa haki za binadamu,usawa wa kijinsia na ukombozi wa wanawake nchini (FemAct) na washirika wengine, wanaandaa Tamasha la Jinsia litalofanyika Septemba.

 

Kwa mujibu wa taarifa ya TGNP iliyotolewa kwa waandishi wa habari na mratibu wake, Eluka Kibona, Tamasha hilo litafanyika kwa siku tatu kuanzia Septemba 13 hadi 16 mwaka huu.

Alitaja malengo ya tamasha hilo la kumi ambalo hufanyika kila baada ya miaka miwili kuwa ni kuibuka, kubadilishana na kuanzisha fikra, uchambuzi wa kutengeneza mikakati ya pamoja ya kudai rasilimali ziwanufaishe wanawake walioko pembezoni.

“Kusherekea nguvu zetu za pamoja, kupanua na kuimarisha ushirikiano katika vuguvugu la ukombozi wa wanawake kimapinduzi na haki ya uchumi katika ngazi ya sekta zoteza kijamii na mengineyo,” alisema Kibona.

Muktadha wa tamasha la mwaka huu kwa mujibu wa TGNP ni kulenga kwenye matamasha ya awali na kujikita katika kuendeleza kampeni kubwa ya haki ya uchumi: ‘Rasilimali ziwanufaishe wanawake walioko pembezoni’.

Pia ni mapambano dhidi ya mfumo dume, sera za kibeberu na mifumo ya utandawazi wakati huu muafaka wa uundaji wa katiba mpya na kusherehekea mika 50 baada ya uhuru wa Tanzania.

“Mada kuu ya tamasha ni Jinsia, Demokrasia na Maendeleo: Ardhi, Ajira na Maisha Endelevu. Lakini vile vile kutakuwa na mada ndogo zitakazotolewa kila siku. Na washiriki ni watu binafsi,vikundi,mashirika,taasisi mbalimbali na mitandao iliyoko katika mapambano yanafanana,” alisema Kibona.

TGNP imewaomba waandishi kuhamasisha jamii kujitokeza kwa wingi kuhudhuria tamasha hilo litakalofanyika katika viwanja vya makao makuu ya mtandao huo jijini Dar es Salaam eneo la Mabibo.