Tamasha la Handeni Kwetu Lawalilia Wadhamini

Mratibu Mkuu wa Tamasha la Handeni Kwetu, Kambi Mbwana akizungumza.

Mratibu Mkuu wa Tamasha la Handeni Kwetu, Kambi Mbwana akizungumza.


 
Na Mwandishi Wetu, Handeni

WADAU wa mambo ya utamaduni yakiwamo mashirika, makampuni na watu mbalimbali wameombwa kujitokeza kuliwezesha tamasha la Handeni Kwetu 2014, lililopangwa kufanyika Desemba 13 mwaka huu wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Tamasha hilo linafanyika huku mwaka jana likiwezeshwa kwa kiasi kikubwa na Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa ushirikiano na wadau mbalimbali walioliwezesha tamasha hilo kwa mara ya kwanza katika Historia ya Mkoa wa Tanga.

Akizungumza mjini hapa, Mratibu Mkuu wa Tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema kuwa wadhamini wakijitokeza kwa wingi kutaongeza chachu ya maendeleo ya nchi, sanjari na sanaa ya utamaduni inayotakiwa kuungwa mkono na watu wengi.

Alisema kuwa kitendo cha wadhamini kuendelea kuliunga mkono Tamasha hilo kutachangia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi wa nchi pamoja na kutangaza utamaduni wa Mtanzania.

“Mwaka jana wadau wengi walijitokeza kuliwezesha tamasha la Handeni, wakiwamo NSSF, hivyo tunaomba msimu huu pia tuendelee kushirikiana kuliwezesha Tamasha la Handeni Kwetu litakalofanyika Desemba 13 mwaka huu, Handeni Mjini.

“Hadi wakati huu, walioonyesha nia ya kulisaidia tamasha la Handeni Kwetu 2014 ni pamoja na SmartMind & Partners iliyopo chini ya Anesa Co. Ltd kwa kupitia kitabu chao cha Ni Wakati wako wa Kung’aa, Phed Trans, chini ya Yusuphed Mhandeni, Handeni Kwetu Foundation, Wait & Watch Film Company Ltd, Qs Mhonda J Apex Group of Companies Ltd na Skyblue Security and Risk Mgt Ltd,” alisema Mbwana.
 
Tamasha la Handeni Kwetu ni miongoni mwa matukio makubwa ya kiburudani mkoani Tanga, ambako zaidi ya watu 500 walihudhuria tamasha hilo ambalo kwa mwaka huu mipango kabambe ya kuhakikisha kuwa linafanyika kwa mafanikio.