Mwandishi Wetu, Moshi
TATIZO la mimba kwa shule za sekondari Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro limetajwa tishio kubwa, kwani ndani ya kipindi cha mwaka 2011 hadi sasa zaidi ya wanafunzi 18 wameripotiwa kutiwa ujauzito na hivyo kukatisha masomo yao.
Taarifa hii imebainishwa na Ofisa Elimu ya Sekondari Manispaa ya Moshi, Bi. Clotilda Mlingi wakati akizungumza na mtandao huu ofisini juu ya kuhusiana na changamoto anuai zinazoikabili sekta ya elimu eneo hilo. Bi. Mlingi amesema takwimu hizo za mwaka 2011 zinaonekana kuongezeka mara mbili yaani kutoka wanafunzi Saba waliopata ujauzito 2010 hadi kufikia wanafunzi 18 mwaka 2011.
“Suala la mimba kwa wasichana katika shule zetu za sekondari bado ni tatizo kubwa linalotukabili kwani pamoja na kuwepo kwa jitihada mbalimbali ambazo tumekuwa tukizifanya tatizo hili limekuwa likizidi kuongezeka badala ya kupungua,” alisema Bi. Mlingi.
Akitaja takwimu kwa kila shule alisema; Shule ya Mjimpya imeonekana kuongeza idadi ambapo kwa mwaka 2010 wanafunzi wawili walifukuzwa kwa kupata ujauzito huku mwaka 2011 wakifukuzwa wanafunzi Watano.
Alisema shule nyingine ambayo inaongoza kwa tatizo hilo ni shule ya Sekondari Msasani ambapo mwaka 2010 kulikuwa hakuna mwanafunzi aliyefukuzwa huku mwaka 2011 wakifukuzwa wanafunzi Wanne, Anna mkapa 2010 Watatu na 2011 wanafunzi Wawili, J. K Nyerere Wanafunzi wawili 2010 na wawili 2011.
Alisema Shule nyingine ni Reginald Mengi ambayo imefukuza mwanafunzi Mmoja 2011, Korongoni wanafunzi wawili huku shule ya msaranga ikiwa haijakumbwa na tatizo hiilo. Alisema tatizo hilo kwa kiasi kikubwa linachangiwa na wazazi kujisahau katika malezi na kuona kuwa jukumu ka kusimamia maadili na nidhamu kwa wanafunzi ni la walimu pekee jambo ambalo si sahihi.
Aidha kiongozi huyo alisema kutokana na tatizo hilo kuendelea kushika kasi wazazi wanapaswa kusimama vema katika nafasi zao na kuhakikisha wanawalea watoto wao katika maadili mema ikiwa niu pamoja na walimu kuendelea kusisitiza na kukazia suala la nidhamu kwa wanafunzi.