Na Aron Msigwa – MAELEZO
OFISI ya Taifa ya Takwimu imesema hali ya mfumuko wa bei nchini imeendelea kuwa katika kiwango kisichobadilika katika kipindi cha mwezi Januari na Februari mwaka huu kutokana na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi, Ephraimu Kwesigabo alisema mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Februari 2014 umeendelea kubaki katika kiwango cha asilimia 6.0 kama ilivyokuwa mwezi Januari mwaka huu.
Alisema kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Februari 2014 imebakia kuwa sawa na ile iliyokuwepo mwezi Januari huku kukiwa na ongezeko dogo la upandaji wa bei kwenye baadhi ya bidhaa na huduma mwezi kwa mwezi Februari 2014 ikilinganishwa na bei za mwezi Februari mwaka jana.
Aliongeza za kuwa mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na migahawa kwa mwezi Februari umeongezeka hadi asilimia 6.9 kutoka asilimia 6.6 za mwezi Januari mwaka huu huku bidhaa zisizo za vyakula kasi ya ongezeko la bei ikipungua hadi asilimia 6.3 mwezi Februari 2014 kutoka asilimia 6.7 za mwezi Januari mwaka jana.
Amefafanua kuwa mwenendo wa bei za bidhaa za vyakula kama samaki, mbogamboga, ulezi na matunda zimeonyesha kuongezeka kwa kiwanga kikubwa kwa mwezi Februar ikilinganishwa na bei za bidhaa hizo kwa mwaka uliopita huku bei za bidhaa zisizo za vyakula za vitambaa vya suti za wanaume, kodi za pango la kuishi, mkaa, na nauli za bajaji zikionyesha ongezeko.
Kwa upande wa mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi,ameeleza kuwa kumekuwa na ongezeko kwa asilimia 1.4 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 1.8 kwa Januari mwaka huu, huku fahirisi za bei za taifa zikiongezeka hadi kufikia 148.62 kati ya Februari mwaka uliopita na Februari mwaka huu.
Amezitaja bidhaa zilizochangia ongezeko la fahirisi za bei nchini kuwa ni pamoja na dagaa, samaki wakavu, mbogamboga na viazi mviringo huku bidha zisizo za vyakula zikiwa pombe za kienyeji, vitambaavya suruali, viatu vya wazi vya plastic, mafuta ya dizeli na Petroli pamoja na huduma za unyoaji na usafi wa nywele.
Aidha kufuatia hali hiyo ya mfumuko wa bei, Kwesigabo ameeleza kuwa uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za jamii kwa mwezi Februari umeonyesha kupungua na kufikia shilingi 67 na senti 29.
“Kupungua kwa thamani ya Shilingi kunamaanisha kwamba, kama mtu alikuwa na uwezo wa kununua bidhaa kwa Shilingi 100 mwaka jana, basi kwa mwaka huu itampasa aongeze zaidi ili aweze kununua kitu kama kile kile, kwa mfano badala ya shilingi 100 inabidi atumie Shilingi 132,”
Kuhusu ulinganifu mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki amesema kuwa una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa mfumuko wa bei nchini Kenya umepungua kidogo na kufikia asilimia 6.86 kwa mwezi Februari kutoka asilimia 7.21 za mwezi Januari, huku Uganda ikiwa na asilimia 6.7 kwa mwezi uliopita kutoka asilimia 6.9 za mwezi Januari.