TAKUKURU wamnasa Kamanda feki wa TAKUKURU Igunga

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Tanzania, Dk. Edward Hoseah.

Igunga

KAMANDA feki wa Tasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Stanley Kimaro ametiwa mbaroni na maofisa wa TAKUKURU mjini Igunga baada ya jamaa huyo kujifanya Kamanda wa tasisi hiyo wa wilaya ya Igunga mitaani.

Kimaro alikuwa akiwapiga mkwara watumishi mbalimbali wa serikali wakiwemo askari Polisi kuwa yeye ni Ofisa TAKUKURU mgeni wa Wilaya hiyo na kuweza kuwatapeli sh.150,000 kwa kutumia cheo hicho.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Kamanda wa TAKUKURU mkoani Tabora, Leonard Mtalai alisema kwamba mtu huyo alikamatwa na maofisa wake, baada ya kupewa taarifa kutoka kwa raia wema juu ya utapeli huo, ambao unalenga kuipaka matope taasisi hiyo kwa wananchi.

Kamanda Mtalai alisema kuwa tukio hilo lilitokea mnamo Julai 6 mwaka huu mjini Igunga majira ya saa 3.30 usiku. Kamanda huyo feki alifanikiwa kuwatapeli Polisi na mhasibu mmoja wa halmashauri ya wilaya hiyo katika mnada, ambapo alimweleza kwamba yeye ni Kamanda mpya wa TAKUKURU wilaya na amefikishiwa taarifa ofisini kwake kuwa ni miongoni mwa watumishi wanaolalamikiwa na jamii kwa kula rushwa.

hivyo kutoka na hali hiyo aliwataka waripoti ofisini kwake mara moja vinginevyo watoe sh. 150,000 ili asiwachulie hatua kali za kinidhamu.

Kutokana na tukio hilo mkuu huyo wa takukuru mkoa amewatahadharisha wananchi na watumishi wa umma kuwa makini na matapeli wanaotumia jina la takukuru kwa kujiita na kujifanya kwamba wao ni maafisa wa takukuru.

Kamanda Mtalai alitaka watumishi wa umma kuwa waangarifu na watu kama hao ambapo alitoa maelekezo kuwaomba vitambulisho vya kazi watu wanaowatilia shaka, na ikibidi kupiga simu kwa tasisi hiyo.

Pia wataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa takukuru kwa kufika au kuwaandikia taarifa sahihi za vitendo vya rushwa vinavyofanywa na watumishi wachache wa umma wasiokuwa waadilifu.