Na Mwandishi Wetu
Karagwe
WANANCHI mkoani Kagera wanaituhumu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwa inajihusisha na vitendo vya kuwalinda wezi wa mifugo kutoka nchi jirani kinyume cha sheria huku wakiweka mbele maslahi yao.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vilivyopatikana wilayani Karagwe hivi karibuni vimemtaja Ofisa wa mmoja wa TAKUKURU (jina tunalo) kuwa amekuwa akiwalinda Wanyarwanda ambao wanashukiwa kuwa ni majambazi sugu wa ngo’ombe katika hiyo na wamekuwa wakiwasaidia kwenye kesi zao.
Taarifa zinafafanua kuwa Septemba 2, 2010 ng’ombe 14 waliibwa wakiwa kwenye zizi la Gosbert Blandes ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Karagwe ambapo ng’ombe watatu walikamatwa kwa Joramu Sebatwale wilaya ya Ngara, ambaye alitambuliwa kuwa ni raia kutoka nchini Rwanda na mtumishi wa Idara ya Mifugo ya Rwanda.
Baada ya kuhojiwa Sebatwale alidai kuwa ng’ombe hao aliwanunua kutoka kwa kutoka kwa mfanyakazi wa mamlaka ya mapato nchini Rwanda na kukanusha kuhusika na wizi wa mifugo kutoka Tanzania.
“Hebu fikiria ndugu mwandishi, unategemia nini ofisa mifugo kutoka nchi jirani anaruhusiwa kujenga zizi katika nchi nyingine na muda wote akituhumiwa kuwa ni mwizi wa mifugo na Serikali inaendelea kukakaa kimya,” alihoji.
Taarifa kutoka katika chanzo hicho zinaeleza kuwa watu wawili waliotwajwa ni Renatus Prospery (26), Mulokozi Itogo (26), ambao wana sadikika kuwa ni raia wa Rwanda na wamekuwa wakitumiwa na ofisa huyo wa TAKUKURU kuiba mifugo Tanzania huku wakichunga mifugo ya ofisa huyo.
Chanzo hicho kilisema watuhumiwa hao waliwahi kupelekwa rumande kwa wakihusishwa na wizi wa mifugo yenye thamani zaidi ya sh. milion 20.5 mali ya Gosbert Blandes kutoka kwenye zizi lililoko Kata ya Ihembe wilayani humo, ambapo walitaka kuipeleka kwenye zizi la ofisa mifugo huyo.
Aidha imeelezwa kuwa ofisa huyo wa TAKUKURU anatuhumiwa kushirikiana na Ofisa Mifugo kutoka nchi ya Rwanda kuwatoa watuhumiwa walioko rumande kwa kutumia hongo kwa mmoja wa mahakimu wa Wilaya ya Karagwe ambaye ndiye aliyekuwa na kesi hiyo.
Uchunguzi uliofanywa na chanzo cha habari hizi unaonesha kuwa gari namba RAB 0061 kutoka Rwanda likiwa ni mali ya mmiliki wa zizi la ng’ombe lililopo Kata ya Ihembe wilayani Karagwe linatumiwa na maofisa hao kufanya shughuli zao.
“Hali hii inatisha kama Watanzania tunaweza kuwapa ushirikiano watu kutoka nje ya nchi kutuibia mali zetu na kuhujumu uchumi, huku watu wengine wakiwa ni watumishi wa umma na wenye dhamana ya kuzuia vitendo vya Rushwa sijui kama nchi yetu itaweza kumudu ushindani wa soko la pamoja la Jumuia ya Afrika Mashariki,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo chanzo juhudi za kumpata Mbunge wa Jimbo la Karagwe kuthibitisha madai hayo ya kuwaachia huru watuhumiwa ambao wanashikiliwa gerezani kutokana na kuwa bungeni na simu yake kuita kwa muda mrefu bila majibu.