Na Sixmund J. Begashe
Mfanyabishara mkubwa wa Chocolate duniani na mmiliki wa Kampuni ya kutengeneza Chocolate nchini Italia, ya SILVIO BESSONO Bw SILVIO BESSONO na ujumbe wake, ameitembelea Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni kwa lengo la kujifunza mambo mbali mbali yanayohusu Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Baada ya kupokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Prof Audax Mabula, Bw Bessono alipata nafasi ya kutembezwa kwenye kumbi zilizo hifadhi Historia ya Tanzania, Sanaa za Mapangoni, Chumba mahususi chenye nyaraka na nyara muhimu, ukumbi wa mila na desturi za watanzania na kisha kumalizia ukumbi wa kisasa wa Maonesho ya sanaa za jukwaani na kisha kuongea na waandishi wa habari.
Katika mazungumzo yake na mwandishi wa habari hizi, Bw Bessono alisema kuwa alikuwa akiisikia tu Tanzania hasa katika uzalishaji wa zao la Cocoa inayosifika sana kwa uzuri duniani, hivyo ikamlazimu kufunga safari hadi hapa nchini kujifunza na kujionea yale aliyokuwa akiyasikia na kuyasoma kwenye machapisho mbali mbali ya kitafiti.
“Nimekuja hapa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni kwa lengo kuu la kujifunza kuhusu Tanzania, watu wake na tamaduni zao, kwa sababu mimi nimefungua milango kwa wakulima wa zao la Cocoa la hapa Tanzania, lakini nimeona nivyema niwafahamu watu hawa vizuri kwa kupitia mwalimu Makumbusho kwani hapa nimejifunza mengi na kwa wakati mfupi” Alisema Bw Bessono.
Bw Bessono aliongeza kuwa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni imemfumbua akili zaidi ya kuutambua ubinadamu wake baada ya kupata historia ya chimbuko la mwanadamu na kujionea fuvu la anaesadikiwa kuwa ni la mwanadamu wa kale alie ishi miaka zaidi milioni 1.7 iliyopita ajulikanae kama Zinjanthropus lililopatikana huko ngorongoro Oldvuvai mwaka 1975.
Akimshukuru Bw Besson kwa kuitembelea Makumbusho, Mkurugenzi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Bw Achiles Bufure amesema ufahamu juu ya umuhimu wa Makumbusho aliouonesha tajiri huyo na mfanya bihashara mkubwa wa Chocolate duniani ni wakuigwa na watu mbali mbali.
“Natoa wito kwa wageni mbali mbali na watanzania wanaotembelewa na wageni kutoka nje ya Tanzania waje kuwatembeza wageni wao Makumbusho ili kuwapa wageni wao fursa ya kujifunza mambo mbali mbali yanayo husu watanzania, maana si rahisi kujifunza mambo ya nchi hii kwa kuizunguka yote lakini wakija hapa watajifunza hata yale yaliyokwisha kutoweka mikononi wa jamii jezetu”.Aliongeza Bw Bufure.
Licha ya kufanya ziara Makumbusho ya Taifa Mfanya biashara huyo mkubwa wa Chocolate duniani aliyatembelea mashamba ya Cocoa yaliyopo Mbingu wilaya ya Ifakara Mkoani Morogoro ili kuongea na wakulina namna ya kuzalisha Cocoa yenye ubora zaidi ambapo yeye ameahidi kulinunua zao hilo kutoka kwa wakulima hao.