TIMU ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhamini na kampuni ya bia ya Kilimanjaro, leo imeanza mazoezi katika uwanja wa Addis Ababa zamani ukifahamka kama (Haille Sellsie) uliopo jijini Addis Ababa kujiandaa na mchezo dhidi ya Misri utakaopigwa Juni 14, jijini Alexandria.
Stars ambayo iliwasili jana jioni jijini Addis Ababa imefikia katika hoteli ya Debre Damo iliyopo eneo na 22 Mazoiria ambapo itakaa kambi kwa kipindi cha wiki moja kujiandaa na mchezo dhidi ya Mapaharao.
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa Stars Mart Nooij amesema anashukuru vijana wake wamefika salama, na wapo katika hali nzuri, anaamini wiki moja ya maandalizi nchini Ethiopia itasaidia kikosi chake kuwa fiti ajili ya mchezo.
Akiongelea kuhusu kambi, kocha Nooij amesema kwa kuwa mji wa Addis Ababa upo katika ukanda wa juu( mita 2000 kutoka usawa wa bahari), kambi ya mazoezi itakua nzuri kutokana na wachezaji kufanya mazoezi katika hali hiyo na kwenda kucheza katika ukanda wa kawaida.
Kuhusu hali ya hewa ni nzuri kwani baridi iliyopo kwa sasa Addis Ababa ni ya kawaida, hivyo haitaweza kuwasumbua wachezaji katika maandalizi ya mchezo dhidi ya Misri.
Mchezo kati ya Misri na Tanzania unatarajiwa kuchezwa katika jiji la Alexandria ambalo lipo eneo la bahari ya Mediteranian.