TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeifunga Harambee Stars ya Kenya bao moja kwa sifuri. Mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa unaotambuliwa na FIFA imefanyika leo jioni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Vijana wa Stars ya Tanzania leo wametoa burudani nzuri kwa wakazi wa Jiji la Mwanza na viunga vyake ikiwa ni kukidhi kilio cha muda mrefu cha kuomba mikoa ya Kanda ya Ziwa ipate nafasi ya kuishuhudia timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ikivaana na timu ya nje.
Wapenzi wa soka wa Kanda ya Ziwa mara kwa mara wamekuwa wakilitupia lawama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa linawanyima nafasi ya kushuhudia mechi za Taifa Stars kwa kuwa mechi nyingi zinafanyika Dar es Salaam au mikoa ya jirani.