TIMU za Taifa za Tanzania (Taifa Stars) na Malawi (The Flames) zinapambana leo Mei 26 mwaka huu katika mechi ya kirafiki itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Makocha wa timu zote mbili, Kim Poulsen wa Taifa Stars na Kinnah Phiri wa The Flames wamezungumzia umuhimu wa mechi hiyo katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika Mei 25 mwaka huu ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kim ambaye hiyo itakuwa mechi yake ya kwanza tangu asaini mkataba wa kuinoa Stars, amesema baada ya mazoezi ya siku kumi hicho ndicho kipimo chake cha kwanza na cha mwisho kabla ya kucheza na Ivory Coast kwenye mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia itakayofanyika ugenini Juni 2 mwaka huu.
“Wachezaji wangu wamekuwa wakipokea mafunzo vizuri ingawa Nurdin Bakari na Thomas Ulimwengu hatakuwepo kwa vile ni majeruhi. Bila shaka baada ya mazoezi ni lazima ujipime, hivyo mechi hii ni muhimu kwangu ukizingatia kuwa kwenye ubora wa viwango vya FIFA, Malawi wako juu yetu,” amesema Kim.
Naye Phiri ambaye ni mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Malawi amesema awali aliombwa mechi na Misri, lakini akaamua kucheza na Taifa Stars kwa vile anaamini kitakuwa kipimo kizuri kwake kabla ya kucheza mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Kenya itakayofanyika Juni 2 mwaka huu jijini Nairobi.
“Nimekuja na wachezaji 20 ambapo nusu yao wanacheza mpira wa kulipwa nje ya Malawi, wengi wakiwa Afrika Kusini lakini wapo pia kutoka Msumbiji na mmoja anacheza Hispania katika timu ya vijana ya Atletico Madrid. Tumejianda si kwa mechi hii tu, bali pia dhidi ya Kenya na baadaye Nigeria ambao tutacheza nao numbani Juni 9 mwaka huu,” amesema Phiri ambaye kwenye benchi lake la ufundi anasaidiwa na Young Chimodzi.
Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 3,000 kwa viti vya kijani, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C na B wakati VIP A inayochukua watazamaji 748 tu itakuwa sh. 20,000.
Wakati huo huo; michuano ya Ligi ya Taifa inayoshirikisha mabingwa wa mikoa inaanza Mei 27 mwaka huu katika vituo vitatu tofauti huku Ashanti United ya Ilala na Polisi ya Mara zikifungua dimba katika Kituo cha Musoma.
Ligi hiyo ambayo inatarajia kumalizika Juni 12 na 13 mwaka huu itashuhudia mechi mbili kwa siku katika kila kituo, huku ya kwanza ikichezwa saa 8 mchana na kufuatiwa nay a pili 10 jioni.
Mechi za ufunguzi Kituo cha Musoma ambapo mechi zake zitachezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma ni Flamingo ya Arusha dhidi ya Forest ya Kilimanjaro (saa 8 mchana) wakati saa 10 jioni ni Ashanti United na Polisi.
Kituo cha Kigoma siku ya ufunguzi kutakuwa na mechi moja tu itakayoanza saa 10 kamili jioni kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika kati ya Mwadui ya Shinyanga na JKT Kanembwa ya Kigoma. Siku inayofuata ni CDA (Dodoma) vs Majimaji ya Tabora (saa 8 mchana) na Bandari ya Kagera vs Pamba ya Mwanza (saa 10 kamili jioni).
Tenende ya Mbeya na Kurugenzi ya Iringa ndizo zitakazoanza saa 8 mchana kwenye Kituo cha Mtwara na kufuatia na mechi kati ya Mpanda Stars ya Rukwa na Ndani ya Mtwara kuanzia saa 10 kamili jioni. Mechi hizo zitachezwa katika Uwanja wa Umoja.