TIMU YA Taifa Stars imepangwa kundi A la michuano ya Kombe la COSAFA ambapo itacheza mechi yake ya kwanza Julai 6 mwaka huu jijini Lusaka, Zambia dhidi ya Shelisheli.
Upangaji ratiba (draw) wa mashindano hayo ulifanyika juzi (Mei 3 mwaka huu) jijini Lusaka ambapo timu nyingine zilizo na Taifa Stars katika kundi hilo ni Namibia na Mauritius. Kundi la Taifa Stars litachezea mechi zake jijini Lusaka.
Mechi ya pili ya Taifa Stars katika hatua ya makundi itakuwa Julai 8 mwaka huu dhidi ya Mauritius. Mechi ya mwisho katika hatua hiyo itakuwa Julai 10 mwaka huu dhidi ya Namibia.
Kundi B lina timu za Kenya (Harambee Stars), Botswana (Zebras), Lesotho na Swaziland. Hatua itakayofuata baada ya hapo ni ya mtoano (knockout) na kila kundi litatoa timu moja tu.
Iwapo Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itafuzu kwa hatua itakayofuata itacheza Julai 13 mwaka huu na Afrika Kusini (Bafana Bafana) ambayo pamoja na timu nyingine tano zimekwenda moja kwa moja katika hatua ya mtoano.
Nyingine zilizokwenda moja kwa moja hatua ya mtoano ni wenyeji Zambia, Angola, Zimbabwe, Msumbiji na Malawi ambazo kwenye viwango vya ubora vya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ziko juu ya zile zilizoanzia hatua ya makundi.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, fainali ya michuano ya Kombe la COSAFA itafanyika Julai 20 mwaka huu.
RATIBA RCL KUPANGWA J’NNE, LIGI KUANZA MEI 12
Upangaji ratiba (draw) ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) uliokuwa ufanyike juzi (Mei 3 mwaka huu), sasa utafanyika Jumanne (Mei 7 mwaka huu) na ligi hiyo itaanza Mei 12 mwaka huu kama ilivyopangwa.
Uamuzi huo umefanya na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana leo (Mei 5 mwaka huu) kujadili maandalizi ya ligi hiyo, yakiwemo maombi ya baadhi ya mikoa ambayo haijamaliza yao kutaka RCL isogezwe mbele.
Kamati ya Mashindano chini ya Uenyekiti wa Blassy Kiondo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF ilipitia maombi hayo na kuangalia athari ambazo zinaweza kujitokeza huko mbele iwapo RCL itasogezwa mbele.
Baadhi ya athari iwapo RCL itasogezwa mbele ni timu zitakazopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutopata muda wa kufanya usajili wa wachezaji kwa msimu mpya.
Hivyo draw hiyo itakayofanyika saa 6 mchana itahusisha mikoa ambayo tayari imemaliza ligi na kuwasilisha majina ya mabingwa wao. Mabingwa ambao wamewasilishwa na mikoa yao kwenye mabano ni Abajalo SC (Dar es Salaam 2), Biharamulo FC (Kagera), Flamingo SC (Arusha), Friends Rangers (Dar es Salaam 3), Katavi Warriors (Katavi), Kiluvya United (Pwani), Kimondo FC (Mbeya) na Machava FC (Kilimanjaro).
Mingine ni Magic Pressure FC (Singida), Mbinga United (Ruvuma), Mji Njombe (Njombe), Polisi Jamii Bunda FC (Mara), Red Coast FC (Dar es Salaam 1), Rukwa United (Rukwa), Saigon FC (Kigoma), TECKFOLT FC ya Kilombero ambayo ni Shule ya Sekondari (Morogoro) na UDC FC ya Ukerewe (Mwanza).
Ada ya ushiriki ni sh. 100,000 wakati usajili wa wachezaji wa timu hizo ni uleule uliofanyika katika Ligi ya Mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF kwa ajili ya uthibitisho. TFF inapenda kusisitiza kuwa hakuna usajili mpya wa wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo.
Mikoa iliyoshindwa kuwasilisha mabingwa wake ni Dodoma, Geita, Iringa, Lindi, Manyara, Mtwara, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Tanga.
AZAM FC KUREJEA NYUMBANI KESHO
Timu ya Azam inatarajiwa kurejea nchini kesho (Mei 6 mwaka huu) saa 7 mchana kwa ndege ya Emirates kutoka Morocco ambapo jana (Mei 5 mwaka huu) ilicheza mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabat ya huko.
Azam ilipoteza mechi hiyo kwa mabao 2-1, hivyo kutolewa katika raundi ya pili ya mashindano hayo. Mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam timu hizo zilitoka suluhu.