Na Anna Nkinda – Maelezo
TAFITI zilizofanyika mwaka 2010 zinaonyesha kila mwaka wanawake 6200 wanakutwa na ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi kati ya hao 4000 wanapoteza maisha kwa kuwa asilimia 10 ya wagonjwa hao wanaweza kuhudhuria Hospitali kwa ajili ya kupata huduma na matibabu. Kutokana na utafiti huo Tanzania ni moja ya nchi yenye wagonjwa wengi wanausumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi ukilinganisha na nchi nyingine zilizopo Afrika ya Mashariki.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Kinga kutoka wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Neema Rusibamayilla wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kutokomeza saratani ya mlango wa kizazi ambayo inafadhiliwa na Muungano wa Utepe wa Pinki, Utepe mwekundu wa nchini Marekani uliofanyika katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam.
Dk. Rusibamayilla alisema ugonjwa wa kansa ni tatizo hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania hii inatokana na sababu mbalimbali zinazozuia watu wasipate vipimo vya ugonjwa hii ikiwa ni pamoja na ukosekanaji wa taarifa za upimaji na utolewaji wa matibabu ya saratani, upatikanaji wa vifaa tiba, utoaji wa huduma, upungufu wa watumishi wa huduma ya afya.
“Naamini mradi huu utaweza kutatua baadhi ya changamoto zinazotukabili kama kuongeza ufahamu kwa jamii kuhusu ugonjwa huu na upatikanaji wa vipimo hii itasaidia kutatuwa tatizo mapema na kupunguza vifo vya wanawake vinavyotokana na ugonjwa huu”, alisema Dk. Rusibamayilla.
Mkurugenzi Mtendaji wa Muungano wa Utepe wa Pinki, Utepe Mwekundu ambao unafanya kazi na Taasisi ya George W. Bush Dk. Doyin Oluwole aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa uongozi wake imara na kuamua kupambana na tatizo la ugonjwa wa saratani na hasa saratani zinazowasumbua wanawake.
Dk. Oluwole alisema, “Katika nchi zote tunazofanya kazi ikiwa ni pamoja na Tanzania malengo yetu ni kuimarisha miundombinu ya afya iliyopo na kufanya kazi na wadau wa afya na hakika tukiungana pamoja na kufanya kazi na watu wengi tutaweza kufika mbali zaidi.
Tuungane kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwani wagonjwa wengi wa saratani ya shingo ya kizazi wako katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya Ugonjwa wa Ukimwi”.
Alisema watafanya kazi na kuhakikisha wanafika nchi nzima hadi vijijini ili kuona wanawake wanapata elimu, vipimo na matibabu na hivyo kuweza kuokoa maisha ya wanawake na wasichana ambao wanasumbuliwa na ugonjwa huo.
Kwa upande wake Dk. Serafina Mkuwa ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) alisema lengo la kuzinduliwa kwa mradi huo ni kuihamasisha jamii ili iweze kufanya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi.
“Tunatoa hamasa kwa wanawake na wasichana wasiogope bali waweze kujitokeza kwa wingi na kupima kwani ukipima na kutokutwa na tatizo utafanyiwa tena uchunguzi baada ya miaka mitatu lakini ukipimwa na kukutwa na ugonjwa unaanza matibabu na ugonjwa huu kama utaanza matibabu mapema utapona”, alisema Dk. Mkuwa.
Naye Mkurugenzi wa Uboreshaji Afya kutoka Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Dk. Sara Maongezi alisema taasisi hiyo imepewa jukumu la kuzungumza na viongozi wa ngazi ya juu wa Serikali kuhusiana na ugonjwa huo.
“Tutaongea na kamati za Bunge za Ukimwi na Ustawi wa jamii ili wakati wa kujadili bajeti ya wizara ya Afya waangaliea zaidi kuhusu saratani na katika ngazi ya mkoa tutawakusanya wataalam wa afya kutoka mikoani na wilayani na kuwapa elimu”, alisema Dk. Maongezi.
Alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni maumivu makali chini ya kitovu, kutokwa na maji machafu ukeni, wakati wa kufanya tendo la ndoa mwanamke atatokwa na damu na mwisho ni damu zinatoka zenyewe bila ya kufanya tendo la ndoa.
Mwezi wa saba mwaka 2013 Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa zamani wa Marekani ambaye pia ni mwanzilishi wa Taasisi ya George W. Bush walizindua Utepe wa Pinki Utepe Mwekundu (PRRR) nchini nia ikiwa ni kuzisaidia nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kupunguza idadi ya wanawake wanaosumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya kizazi na matiti.
Utepe wa Pinki Utepe Mwekundu ulitoa dola za Marekani milioni 1.2 fedha ambazo zitatumika katika mradi huo ambao kwa mara ya kwanza utaanza katika mikoa ya Mbeya, Mwanza na Iringa. Kampeni hiyo inafanywa chini ya usimamizi wa wizara ya Afya na Ustawi wa jamii kwa kushirikiana na muungano wa Utepe wa Pinki Utepe Mwekundu, Taasisi ya WAMA, MEWATA, T-MARC,TAYOWA na Mtandao wa kupambana na ugonjwa wa Ukimwi Mkoani Mbeya.