Na Anitha Jonas – MAELEZO
SHIRIKISHO la Filamu Tanzania laanda Tamasha la Tuzo za Filamu (TAFA) linalotarajia kufanyika Mwezi Mei 2015 katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam lenye lengo la kuonyesha wachezaji filamu chipukizi wanaofanya vizuri katika tansia ya filamu nchini.
Hayo yamesemwa na Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania Bw. Simon Mwakifwamba alipotembelewa ofisini kwake na Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu nchini Bibi Joyce Fisoo kwa ajili ya kujua maendeleo ya maandalizi ya Tamasha hilo lenye nia ya kukuza tansia ya filamu nchini na kudhamini mchango wa filamu katika kuongeza kipato kwa vijana, kuelimisha na kuburudisha jamii.
“Tuzo hizi zitakuwa na majaji wenye uzoefu mkubwa kutoka Afrika Mashariki ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda na Tanzania na pia ushindani umegawanyika katika vigezo kumi na tatu na washindani katika vigezo hivyo ni kati ya wasanii watano mpaka nane ambapo kwasasa namba ya kuwapiga kura washiriki hao kwa njia ya simu imeshapatikana na mchakatao wa kupanga namba za washiriki kulingana na vigezo vyao wanavyoshindania vinaendelea na mchakato huo utakamilika hivi karibuni,” alisema Bw. Mwakifamba.
Rais wa Shirikisho hilo aliendelea kusema kuwa maandalizi ya tuzo hizo yamekuwa na changamoto kubwa ikiwemo ukosekanaji wa fedha za kutosha na ufadhili hivyo ombi lake kwa watanzania wote na wadau mbalimbali kujitokeza kutoa ufadhili katika kufanikisha utolewaji wa tuzo hizo kwani ni jambo lenye manufaa kwa wasanii wa filamu kutokana na kazi nzuri ya kuburudisha na kuelimisha jamii hivyo ni vyema tutambue mchango wao.
Aidha Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi Joyce Fisoo alimsihi Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania kuandaa mwongozo wa kutengeneza video za kampeni ya uhamasishaji wa tuzo hizo na kuziwasilisha ofisi ya Bodi ya Filamu kuzihakiki na kuandaa namba maalum ya mitandao ya simu ambayo wananchi wanaweza kutuma michango yao kupitia M-PESA, TIGOPESA, AIRTEL MONEY na EZY PESA kwa ajili ya kufanikisha tamasha hilo.
“Ni vyema muwe mnaleta taarifa fupi Wizarani kuhusu maandalizi ya tuzo hizo ili uongozi ujue namna gani mmejipanga na maandalizi yanakwenda vipi na Serikali iwasaidie wapi ili kufanikisha tamasha hilo na kwa kufanya hivi mnaweza kupata ushauri na maelekezo muhimu ya kuzingatia katika maandalizi hayo,” alisema Bibi Fisoo.
Halikadhalika Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu aliwataka viongozi wa Shirikisho la Filamu nchini kuwa na mshikamano miongoni mwao ili kuweza kufanikisha tamasha hilo kwani Umoja ni nguvu hivyo kufanya kazi kwa umoja.