Na Hassan Silayo – MAELEZO
MAWAKALA wa Forodha nchini wameaswa kujisajili katika mfumo wa uondoshaji mizigo wa Himaya moja ya Forodha ya Afrika Mashariki (Single Custom Territory) utakao anza kutumika hivi Karibuni. Hayo yamesemwa na Kamishna wa Forodha Kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Tiagi Kabisi wakati mkutano na Viongozi na wanachama wa Chama cha Mawakala wa Forodha (TAFA).
Bw. Kabisi alisema kuwa mawakala wa forodha nchini hawana budi kufanya hivyo ili kuwezesha uondoshwaji wa mizigo kwa haraka zaidi pindi mfumo huo utakapoanza kutumika.
“Sasa tunaelekea katika matumizi ya Himaya moja ya Forodha ya Afrika Mashariki yaani Single Custom Territory ili kuwa na uwezo wa kupata huduma kwa kutumia mfumo huo pindi matumizi yatakapoanza mapema ili kuondoa usumbufu utakaoweza kutokea,” alisema Bw. Kabisi.
Bw. Kabisi aliongeza kuwa mpaka sasa ni makampuni mawili (2) ya mawakala waliojisajili mpaka sasa.
Aidha Bw. Kabisi alisema kuwa mawakala wa forodha hawana budi kuendelea kuwa waamifu ili waendelee kuongoza katika makusanyo ya fedha kwa mwaka ujao ambapo kwa mwaka huu wamechangia kwa asilimia 40 ya mapato ya serikali.
Naye Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha (TAFA) Bw. Stephen Ngatunga alisema kuwa wataendelea kushirikiana na Mamlaka la Mapato Tanzania (TRA) katika kuhakikisha wanaifanya idara ya forodha inafanya vizuri katika makusanyo ya fedha. Pia Bw. Ngatunga aliitaka serikali kuendelea kushughulikia changamoto mabalimbali zinazoikabili idara hiyo ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu na kuendelea kuongoza katika makusanyo ya mapato ya Serikali.