JAMII imetakiwa kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia watoto na wazee ikiwa na pamoja na viongozi wa dini kuzitumia nafasi zao kukomesha ukatili huo. Akifungua katika mkutano wa wadau uliowashirikisha viongozi wa dini na wadau mbalimbali kutoka Wilaya ya Pangani, Lushoto, Handeni na Tanga mjini kupitia mradi wa GBV, Mkurugenzi wa Tree of Hope, Fortunata Manyeresa, alisema viongozi wa dini wako na nafasi kubwa ya kutokomeza ukatili wa kijinsia maeneo yao.
Alisema vitendo vya ukatili vya kijinsia vimekuwa vikishamiri kila siku hivyo kuwataka viongozi hao wa dini kutumia nafasi zao katika jamii kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa.
“Jambo la kufurahisha hapa leo tupo na viongozi wa dini tofauti pamoja na wanaharakati, tutumie nafasi zetu kwa kukemea vitendo vya ukatili” alisema Manyeresa na kuongeza.
“Bado ukatili wa kijinsia kwa watoto na wazee unaendelea hili ni jambo la kuhuzunisha na linatakikana kupingwa kwa nguvu zote kwa kushirikiana na Serikali,” alisema.
Afisa mradi Tree of Hope, Goodluck Malilo, aliwataka wanaharakati kutoka Wilayani kuwa mabalozi wa kupambana na vitendo vya ukatili watoto na wazee. Alisema kwa kupaza sauti moja vitendo hivyo vinaweza kutokomezwa hivyo kuwataka baada ya kupata maelekezo na mbinu kuhakikisha wanawafikisha katika vyombo vya sheria wote wanaojihusisha na ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wake Mwanaharakati kutoka Wilayani Mkinga, Fidea Mtambo alisema vijijini kuna changamoto kubwa ya kupambana na vitendo vya kikatili hivyo kuitaka Asasi hiyo kuendeleza mapambana yake kijiji kwa kijiji.
Naye Ustadhi, Ustadhi Abdalla Mbena kutoka kata ya Donge Tanga mjini, alisema kuna baadhi ya watu wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia wamekuwa waoga kutoa taarifa kwa vyombo vya dola. Alisema ili kuweza kutokomeza ni wajibu wa kila mmoja kuwa balozi wa kupinga vitendo vya ukatili vya kijinsia katika eneo lake.