Taarifa za TFF Septemba 11, 2012

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura

Taarifa za TFF Septemba 11, 2012

KAMATI ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana jana (Septemba 10 mwaka huu) ili kupitia na kutoa uamuzi/ushauri kwa masuala mbalimbali yaliyowasilishwa mbele yake.

Wajumbe sita kati ya saba waliopo walihudhuria kikao hicho chini ya Mwenyekiti Alex Mgongolwa. Wajumbe hao ni Hussein Mwamba, Imani Madega, Ismail Aden Rage, Llyod Nchunga na Omari Gumbo.

Suala la ugombea wa Michael Wambura katika FAM
Michael Wambura aliomba uongozi katika Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM) katika uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka jana. Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliondoa jina lake kwa kukosa sifa ya kugombea nafasi hiyo.

Wambura hakuridhika na uamuzi huo akapeleka shauri lake Kamati ya Nidhamu ya TFF. Kamati hiyo katika uamuzi wake ilisema haina mamlaka ya kushughulikia shauri hilo. Baadaye Wambura alikata rufani katika Kamati ya Rufani ya TFF ambayo ilimpa haki ya kugombea.

Kutokana na mkanganyiko huo wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwa na uamuzi wa mwisho katika masuala ya uchaguzi ya wanachama wa TFF, na uamuzi wa Kamati ya Rufani kuhusu uchaguzi wa mwanachama wa TFF, Sekretarieti ya TFF iliomba mwongozo wa kisheria kwa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji.

Kwa vile Kamati hizo mbili (Uchaguzi na Rufani) haziko katika mtiririko wa moja kwa moja wa utoaji maamuzi, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji iliishauri Sekretarieti ya TFF kuliandikia Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ili kupata muongozo juu ya suala hilo.

Katika muongozo wake, FIFA ilitoa maoni kuwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF chombo cha mwisho cha rufani katika masuala ya uchaguzi kwa wanachama wa TFF ni Kamati ya Uchaguzi ya TFF. Hata hivyo, FIFA ilishauri kuwa si vizuri chombo kimoja kikawa msimamizi wa uchaguzi, na chenyewe tena ndiyo kiwe cha mwisho katika uamuzi kwenye uchaguzi husika.

Hivyo, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji imetoa mapendekezo mawili kwenda Kamati ya Utendaji kwa ajili ya marekebisho ya Katiba ili kiwepo chombo kingine cha rufani pale mgombea anapopinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF.

Mapendekezo hayo ni; Iundwe Kamati ambayo itakuwa inasikiliza rufani zote zinazotokana na uamuzi uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, hivyo Kamati ya Uchaguzi ya TFF isiwe chombo cha mwisho cha uamuzi kwa rufani zinazotokana na uchaguzi wa wanachama wa TFF.

AU. Rufani zote zinazotokana na uchaguzi wa wanachama wa TFF zisikilizwe na Kamati ya Rufani ya TFF. Kwa maana hiyo Kamati ya Rufani ya TFF ndiyo kiwe chombo cha mwisho kwa wasiokubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwasilisha malalamiko yao.

USAJILI/PINGAMIZI DHIDI YA WACHEZAJI

Musa Hassan Mgosi, Ayoub Hassan Isiko
Mchezaji Musa Hassan Mgosi ameombewa usajili Ruvu JKT kutoka DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), na Ayoub Hassan Isiko ameombewa usajili Mtibwa Sugar kutoka Bull FC ya Uganda. Wachezaji hao hawaruhusiwi kuchezea timu hizo mpaka Hati zao za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) zitakapokuwa zimepatikana.

Toto dhidi ya Kagera Sugar kumsaini Enyinna Darlinton Ariwodo
Toto Africans ilipinga usajili wa Enyinna Darlinton kwa timu ya Kagera Sugar kwa vile bado ina mkataba wa mchezaji huyo ambao unamalizika mwakani.

Kwa upande wake Kagera Sugar ilisema imemsaini mchezaji huyo kwa vile Toto Africans imeshindwa kumlipa mshahara ambapo kuna makubaliano rasmi kati ya Ariwodo kuwa klabu hiyo ikishindwa kumlipa mshahara anaruhusiwa kuondoka.

Uamuzi wa Kamati ni kuwa Ariwodo ni mchezaji halali wa Kagera Sugar kwa vile Toto Africans ilishindwa kutimiza masharti ya mkataba.

Ramadhan Chombo ‘Redondo’
Redondo ameidhinishwa kuchezea Simba kwa kuzingatia mchezo wa haki na uungwana (Fair Play) baada ya klabu hiyo na ile ya Azam kufikia makubaliano kuhusu mchezaji huyo.