Taarifa za Soko la Ajira Zahitajika Kupanga Matumizi ya Nguvu kazi

Msemaji wa Wizara ya Kazi na Ajira Ridhiwani Wema alibainisha kuwa ajira zilizalishwa katika maeneo makuu mawili

Msemaji wa Wizara ya Kazi na Ajira Ridhiwani Wema alibainisha kuwa ajira zilizalishwa katika maeneo makuu mawili

Na Benedict Liwenga, Maelezo-DSM.

Taarifa za soko la ajira zina umuhimu wa kipekee katika kupanga, kutekeleza na kupima ufanisi wa mipango ya kiuchumi nchini pamoja na kupima uwezo wa kiuchumi kwa wakati husika, hivyo taarifa hizo ni miongoni mwa vigezo vikuu vinavyotoa picha halisi ya mafanikio ya kiuchumi na kimaendeleo kwa nchi au mahali husika.

Wizara ya Kazi na Ajira ni moja ya Wizara yenye jukumu la kuratibu utekelezaji wa Sera, Sheria na Mikakati ya kukuza ajira pamoja na kutoa taarifa hizo kuhusu mwenendo wa Soko la Ajira nchini.

Taarifa toka katika Wizara hiyo zinaeleza kwamba, katika kipindi cha miezi mitatu yaani Julai hadi Septemba, 2014 jumla ya ajira 139,361 zimezalishwa, hivyo kupelekea kasi ya uzalishaji wa nafasi za ajira nchini kuzidi kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Msemaji wa Wizara ya Kazi na Ajira Ridhiwani Wema alibainisha kuwa ajira zilizalishwa katika maeneo makuu mawili yakiwemo ya Ajira Serikalini ambayo ni 3,657 sawa na asilimia 2.6% na ajira kupitia sekta binafsi ambayo ni 135,704 sawa na asilimia 97.4%.

Wema alisema kuwa, kasi ya ongezeko la nafasi za kazi katika sekta rasmi binafsi imekua ikiongezeka mwaka hadi mwaka kuanzia mwaka 2011/2012 sambamba na ukuaji wa uchumi ambapo kwa mwaka 2011/2012 jumla ya ajira 250,678 zilizalishwa hiyo ni sawa na asilimia 6.4%, pia kwa mwaka 2012/2013 jumla ya ajira 274,030 zilizalishwa sawa na asilimia 6.9% na mwaka 2013/2014 zilizalishwa ajira 408,756 sawa na asilimia 7.0%, mathalani mwaka 2014/2015 jumla ya ajira 560,000 zinatarajiwa kuzalishwa katika sekta binafsi rasmi, na hii inaonyesha ongezeko zaidi la soko la ajira nchini.

Alifafanua kuwa, katika mwaka 2013/2014 sekta binafsi rasmi ambayo ndiyo mwajiri mkuu, iliweza kuzalisha jumla ya ajira 408,756 kupitia uwekezaji katika maeneo mbalimbali yakiwemo; Viwanda vidogo na kati (SMEs) ajira 7,192 sawa na asilimia 1.6, Uwekezaji kupitia SEZ na EPZ ajira 26,381 sawa na asilimia 6%, Uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) ajira 149,594 sawa na asilimia 34.2%, Sekta ya Mawasiliano ajira 13, 619 sawa na asilimia 3.1 na Sekta nyinginezo ajira 240,147 sawa na asilimia 55.

“Utafiti wa Ajira na Mapato (Employment and Earning Survey) wa mwaka 2013 umeonyesha ajira ya watu wenye ulemavu ni asilimia 0.3 ya ajira zote zilizozalishwa katika sekta rasmi binafsi”, alisema Wema.

Akiitaja baadhi ya Mikoa yenye kutoa ajira hizo, alisema kuwa, mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kutoa ajira nyingi rasmi ambayo ni sawa na asilimia 30 ikifuatiwa na Mikoa ya Morogoro wenye asilimia 10.7%, Arusha asilimia 6.6%, Kilimanjaro asilimia 5.8%, Mbeya asilimia 5.8 na mkoa ulioajiri watu wachache ni mkoa wa Katavi wenye asilimia 0.1%.

“Utafiti huu umeonyesha kuwa viwango vya mishahara katika sekta rasmi vimeimarika ambapo zaidi ya asilimia 30 ya Wafanyakazi katika sekta rasmi binafsi wanapata mshahara unaozidi shilingi 500,000 ikilinganishwa na mwaka 2012 ambapo asilimia 25.2% walipata mishahara zaidi ya kiwango hicho”, aliongeza Wema.

Aidha, katika taarifa hiyo aliyoitoa Msemaji wa Wizara hiyo ilionyesha kuwa walioajiriwa wengi ni zaidi ya asilimia 41% ambapo walikuwa na elimu ya kati Diploma ama Diploma ya juu na asilimia 19% Elimu ya Juu yaani Shada ya kwanza na zaidi.

Halikadhalika, waajiriwa wengi zaidi ya asilimia 28.0% waliajiriwa katika sekta ya Uzalishaji (Manufacturing), asilimia 11.3% katika kilimo, asilimia 10.2% katika biashara na asilimia 2.3% katika huduma za fedha na bima.

Alisisitiza kuwa, Takwimu hizo zinaonyesha sekta binafsi itafanya vizuri zaidi endapo Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya waajiri kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania.

Aidha, alifafanua kwamba hatua zinazochukuliwa sasa ni pamoja na kufanya marekebisho ya Sera ya Ajira ya mwaka 2008, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya Na. 6, 2004, Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7, 2004 pamoja na kutunga Sheria Mpya ya Ajira za Wageni nchini ambayo imelenga kulinda ajira za Watanzania, kuboresha Mzingira ya Biashara na kuhamasisha uwekezaji.

Rai ya ushirikiano kwa waajiri wote nchini ilitolewa katika zoezi zima la kukusanya taarifa za soko la ajira licha ya kuwepo baadhi ya wadau wenye kutoa taarifa hizo kwa wakati.

“Taarifa hizi ni kwa lengo la kuiwezesha serikali kujua hali ya ajira nchini na kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuwezesha serikali kupanga matumizi sahihi ya nguvukazi nchini”, aliongeza Wema.