WAGANDA KUCHEZESHA NGORONGORO VS SUDAN
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limewateua waamuzi kutoka Uganda kuchezesha mechi ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 kati ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) na Sudan itakayofanyika Aprili 21 mwaka huu.
Mwamuzi atakayechezesha mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni ni Brian Miiro. Waamuzi wasaidizi ni Mark Ssonko na Lee Patabali wakati mwamuzi wa mezani ni Denis Batte.
Ejigu Ashenafi wa Ethiopia ndiye ameteuliwa kuwa Kamishna wa mechi hiyo namba 15. Kamishna na waamuzi hao watawasili nchini Aprili 19 mwaka huu kwa ndege za Ethiopian Airlines na Air Uganda.
KINYANG’ANYIRO VPL KUENDELEA APRILI 18
Kinyang’anyiro cha Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara kinaendelea tena kesho (Aprili 18 mwaka huu) kwa mechi tano zitakazochezwa kwenye miji ya Bukoba, Mwanza, Dar es Salaam, Mlandizi na Dodoma.
Mabingwa watetezi Yanga watakuwa wageni wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba wakati Toto Africans itaikaribisha African Lyon kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Vinara wa ligi hiyo Simba wataoneshana kazi na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Ruvu Shooting na Moro United zitaumana kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi. Nayo Polisi Dodoma itakuwa mwenyeji wa Coastal Union mjini Dodoma.
TENDA YA TIKETI KUFUNGULIWA APRILI 18
Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kesho (Aprili 18 mwaka huu) itafungua maombi ya tenda zilizowasilishwa na kampuni mbalimbali kwa ajili ya kutengeneza tiketi za elektroniki.
Maombi hayo yatafunguliwa saa 9 alasiri kwenye ofisi za TFF ambapo kampuni zote zilizowasilisha tenda zinatakiwa kuwepo wakati wa ufunguzi huo.
Machi 9 mwaka huu TFF ilitangaza tenda kwa ajili ya kutengeneza tiketi za elektroniki kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom na mechi nyingine inazozisimamia.
SIMBA, SHOOTING ZAINGIZA MIL 40/-
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Ruvu Shooting na Simba lililochezwa juzi (Aprili 15 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 40,855,000.
Jumla ya watazamaji 10,824 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa viingilio vya sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 15,000. Watazamaji 8,500 kati ya hao walishuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 3,000.
Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 6,232,118.64 kila klabu ilipata sh. 7,406,424.41, uwanja sh. 2,468,808.14.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 2,468,808.14, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 493,761.63 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) sh. 493,761.63.
Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,234,404.07, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 246,880.81 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni sh. 2,468,808.14.
Gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000 na nauli ya ndani kwa mtathmini wa waamuzi sh. 10,000.
Mwamuzi wa akiba sh. 30,000, posho ya kujikimu kwa kamishna, mtathmini wa waamuzi na waamuzi sh. 200,000, gharama ya tiketi sh. 2,460,000, maandalizi ya uwanja (pitch) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000.
Gharama nyingine ni Jichangie ambayo ni sh. 200 kwa kila tiketi; kila klabu ilipata sh. 757,680 wakati Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata sh. 649,440.
Nayo mechi kati ya Villa Squad na Coastal Union iliyochezwa Aprili 15 mwaka huu kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam iliingiza sh. 499,000 ambapo kila klabu ilipata sh. 44,374 wakati watazamaji walioshuhudia mechi hiyo ni 451.
Vilevile mechi kati ya Moro United na JKT Oljoro iliyochezwa Aprili 14 mwaka huu Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam iliingiza sh. 410,000 kutokana na washabiki 402. Kila klabu ilipata sh. 39,257.
7,186 WASHUHUDIA MECHI YA TOTO AFRICANS, YANGA
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Toto Africans na Yanga iliyochezwa juzi (Aprili 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ilishuhudiwa na watazamaji 7,186 na kuingiza sh. 15,392,000. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000 kwa jukwaa kuu na sh. 2,000 mzunguko.
Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 2,347,932 kila klabu ilipata sh. 2,729,060, uwanja sh. 909,686.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 909,686, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) sh. 363,874, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 454,843, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 90,968 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni sh. 909,686.
Gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000. Mwamuzi wa akiba sh. 30,000, posho ya kujikimu kwa kamishna na waamuzi sh. 160,000, gharama ya tiketi sh. 2,300,000.
Gharama nyingine ni Jichangie ambayo ni sh. 200 kwa kila tiketi; kila klabu ilipata sh. 503,020 wakati Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) kilipata sh. 431,160.
MTWARA FA WAPATA VIONGOZI WAPYA
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA) kimepata viongozi wapya katika uchaguzi uliofanyika juzi (Aprili 15 mwaka huu) ukumbi wa Clinical Officers Training College wilayani Masasi.
Waliochaguliwa ni Athumani Kambi (Mwenyekiti), Vincent Majili (Katibu Mkuu), Kazito Mbano (Mhazini) na mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Fredrick Nachinuku.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa MTWAREFA walikuwa 30 ambapo Kambi alipata kura 23 za ndiyo na saba za hapana wakati Majili alipata kura 27 dhidi ya tatu za Charles Haule.
Nafasi nyingine hazikuwa na wagombea ambapo uchaguzi mdogo utaitishwa baadaye.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)