Sweden Kuendelea Kukuza Ushirikiano na Tanzania

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi mkuu wa SIDA Bw. Torbjorn Petterson makao makuu ya shirika hilo la maendeleo la Sweden jijini Stockholm

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi mkuu wa SIDA Bw. Torbjorn Petterson makao makuu ya shirika hilo la maendeleo la Sweden jijini Stockholm

Na Premiere Kibanga, Stockholm, Sweden
NCHI ya Sweden imedhamiria kuukuza ushirikiano wake na Tanzania kwa Awamu mpya ambayo itaongeza uwekezaji na biashara zaidi. Rais na Mtendaji Mkuu wa Muungano wa wafanyabiashara wa Sweden, Business Sweden, Bi Ylva Berg amemueleza Rais Kikwete katika mkutano wa Business Sweden na Rais Kikwete, Juni 5, 2015 katika Kituo cha Biashara (World Trade Centre) jijini Stockholm.

“Tunataka kushirikiana, kufanya biashara na uwekezaji na Tanzania hapa kwenye masuala ya nishati” amesema Bi Berg.
Sweden inachangia dola bilioni 1 katika Mfuko wa Nishati wa Rais Barack Obama wa Marekani maarufu kama Power Africa, ambao unalenga katika kuongeza idadi ya watu wanaotumia umeme barani Afrika.

Mpango huo unaanza kwa Nchi 6 ambazo ni Tanzania, Ethiopia, Ghana, Liberia, Kenya na Nigeria. Katika mkutano huo Rais Kikwete amewaeleza wafanyabiashara hao ambao pia ni wamiliki wa makampuni makubwa ya kimataifa kuwa sekta ya Nishati ni sekta inayokua kwa haraka sana nchini Tanzania.
“Tunahitaji wenza katika kukuza sekta ya Nishati, serikali haiwezi Peke yake”. Rais amesema na kuwaeleza mahitaji ya nishati yaliyopo Tanzania na Nchi za jirani.

Rais Kikwete pia amefanya mazungumzo na Waziri wa Nyumba, Maendeleo ya Jiji na Mawasiliano Bw. Mehmet Kaplan, ambaye naye amefuatana na wafanya biashara wakubwa wa Sweden ili kupata picha kamili ya maendeleo na uwekezaji nchini Tanzania. Rais ameelezea fursa zilizopo na kutoa changamoto kwa wafanyabiashara hao kuja kuwekeza Tanzania ili kuinua uchumi, kukuza ajira na hatimaye kuifanya Tanzania iweze kujitegemea na kuondokana na bajeti tegemezi.

Rais amemaliza ziara yake nchini Sweden kwa kutembelea Chuo cha Afya cha Karolinska ( Karolinska Institute ) ambacho kinashirikiana na Chuo cha Afya Muhimbili kwa zaidi ya miaka 20 sasa ambapo wataalamu wake kwa pamoja wanashirikiana katika shughuli za utafiti katika masuala ya Malaria na HIV.

KI Kama kinavyojulikana, zaidi ni Chuo cha 3 kwa ukubwa nchini Sweden na kinaongoza katika masuala ya utafiti. Mbali na ufadhili na ushirikiano na Muhimbili, KI pia inafanya utafiti kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar, ambapo juhudi zao kwa pamoja zimeweza kuondosha Malaria Zanzibar. Rais Kikwete anatarajia kuondoka Usiku wa jana ambapo anatarajia kuanza ziara ya kikazi ya siku 3 nchini Uholanzi.