Swahili Fashion Week ya Sita Yazinduliwa, Wabunifu 40 Kuonesha Kazi Zao Dar

IMG_0598

 

Waandaaji wa Swahili Fashion Week wakizungumza waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

IMG_0604

 

Meneja Mawasiliano, wa Swahili Fashion Week, Kauthar Ally (aliyesimama) akizungumza na waandishi wa habari juu ya  Maonesho ya Sita ya Swahili Fashion Week.

 

 

IMG_0584

IMG_0576

 

Pichani juu baadhi ya Waandaaji Maonesho ya Sita ya Swahili Fashion Week na wanahabari Golden Tulip Hotel.

Na Mwandishi Wetu

MAONESHO ya Sita ya Swahili Fashion Week yanatarajiwa kuzinduliwa kuanzia Desemba 5 na kufanyika hadi Desemba 8 2013. Maonesho hayo kabambe yanatarajiwa kufanyika katika Hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam katika Hoteli ya Golden Tulip, Meneja Mawasiliano Kauthar Ally alisema jumla ya wabunifu 40 kutoka ndani na nje ya Tanzania wanatarajia kuonesha kazi zao hivyo kuwataka Watanzania na wadau wote kujitokeza kuunga mkono kazi za wabunifu wa Tanzania.

Alisema kazi ambazo zinatarajiwa kuoneshwa zimeandaliwa kwa ufasaha na zinakwenda na wakati hivyo kazi hizo zinategemewa kushika soko la Afrika Mashariki kwa mwaka 2014.

“Swahili Fashion Week mwaka huu ina lengo la kuifikia jamii zaidi, na kukuza vipaji katika tasnia ya mitindo. Ni zaidi kuhusu kuthamini wabunifu wa kwetu na kuwatengenezea jina, huku tukiwapeleka ngazi za juu zaidi kila mwaka,” aliongeza Washington Benbella, Meneja wa Swahili Fashion Week.

Alisema mwaka huu ambao ni wa sita katika mashindano ya wabunifu wanaochipukia, waandaaji wamependekeza dhima ya maonesho kuwa ‘Evolution’, ambayo inawataka wabunifu chipukizi kubuni mavazi yanayoashiria mabadiliko, si lazima upya lakini muonekano wake uwe tofauti na mzuri zaidi.

“Kimsingi tunasisitiza jamii iunge mkono tasnia ya mitindo na kuvaa mavazi ya kikwetu hasa kwa Tanzania. Vipaji vya nyumbani vinaitaji kukuzwa ili kufikia majina makubwa yanayotambulika duniani kupitia tasnia hii. Hisani huanza nyumbani na ndio maana tunategemea kampuni pamoja na mashirika mbalimbali kusaidia tasnia ya mitindo,” aliongeza Meneja Masoko wa Swahili Fashion Week, Hamis Omary.

Swahili Fashion Week imedhaminiwa na EATV, East Africa Radio, Golden Tulip Hotel, Eventlites, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Ultimate Security, Global Outdoor Ltd na 361 Degrees.