Superbrand kuzitangaza bidhaa zinazofanya vizuri 2011

Mkurugenzi wa Superbrand Mradi wa Afrika Mashariki, Jawad Faffer akiwapa nembo ya Superbrand ya ushindi, Meneja wa Maendeleo ya Bidhaa na Utafiti, Benki ya CRDB (kushoto) na Daniel Hill Meneja Mauzo na Biashara wa Azam (kulia) mara baada ya kuwatangaza washindi kupitia bidhaa/huduma zao leo Dar es Salaam. (Picha na Joachim Mushi)

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Utambuzi wa Bidhaa zinazofanya vizuri ya Superbrand imesema mwezi ujao inatarajia kufanya hafla ya mwaka ikiwa ni hatua ya kuzitangaza na kuzipa heshima bidhaa zinazofanya vizuri sokoni.

Akizungumza katika taarifa yake aliyoitoa leo jijini Dar es Salaam, wakati akizitaja kampuni ya Azam pamoja na Benki ya CRDB zilizofanya vizuri katika bidhaa zao kadhaa, Mkurugenzi wa Mradi wa Afrika Mashariki, Jawad Faffer amesema SuperBrand imezamiria kuzitambua bidhaa zinzofanya vizuri.

Amesema SuperBrand mbali na kuzitambua bidhaa hizo pia itaendelea kutoa ushauri wa kitaalamu kwa kampuni husika ili kuhakikisha zinaongeza ubora ikiwa ni pamoja na kufanya vizuri hatimaye kuongoza duniani.

Alisema sifa iliyonayo mamlaka ya ya Superbrand inaendelea kuziongezea bidhaa husika thamani na kuwashinda washindani wengine sokoni. “Programu hii inaongozwa na kamati iliyojitolea ikiongozwa na wataalamu waliobobea wanaotambua mipaka ya bidhaa ambazo zinakuwa zinafanywa uchunguzi sahihi,” alisema Faffer.

Aidha akifafanua zaidi Faffer alisema, Superbrand imeanzisha programu zake kwa zaidi ya nchi 88 duniani ikiwa ni pamoja na masoko makubwa duniani. Mojawapo ya masoko hayo makubwa duniani ni pamoja na Mercedes Benz, Coca Cola, BMW, Google na Microsoft.

Alisema kampuni yake inafarijika kuendelea kuziona bidhaa imara zinafanya vizuri kwenye soko la Afrika Mashariki, kwani bidhaa hizo mbali na kupitishwa na wanakamati wa Superbrand pia zilipigiwa kura na wateja zaidi ya 2500 ambao walipiga kura za papo kwa papo.