Sumaye: Epukeni Wanaotoa Fedha kwa Kutumia Mgongo wa Dini

Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye

WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amewataka viongozi wa dini na Watanzania kwa jumla kuwa makini na watu wanaojipitisha na kutoa fedha kutaka uongozi akisema hiyo imezaa matabaka kwa wanyonge kukosa haki za msingi kwa kuwa hawana fedha.

Sumaye alisema hayo jana kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), zilizofanyika Chuo Kikuu cha Makumira, Arumeru.

Mbele ya Maaskofu wote 20 wa Dayosisi zote za KKKT nchini na wageni waalikwa kutoka ndani na nje ya nchi, Sumaye alisema jeuri ya fedha na mamlaka imesababisha mambo mengi machafu katika jamii ikiwamo wanyonge kukosa haki zao za msingi, huku wenye uwezo kifedha wakipata haki kwa kutoa hongo au rushwa.

Alisema hali imekuwa mbaya kiasi kwamba hata nafasi za uongozi hivi sasa zinapatikana pasi na kuzingatia uwezo kiutendaji na uadilifu wa mhusika na badala yake kinachoangaliwa ni mhusika anayeomba uongozi ametoa fedha kiasi gani za kuwahonga wapiga kura.

“Hata katika baadhi ya dayosisi na sharika zetu watu wamekuwa wakipewa sifa za ajabu si kwa sababu ya uadilifu wao au wema wao, bali kwa sababu tu wamechangia fedha kwa shughuli zetu za kanisa au hata binafsi,” alisema.

Aliwataka viongozi wa kidini kutojielekeza kwenye huduma za kiroho pekee, bali washughulike na mambo yote yanayoikwaza jamii wanayoiongoza ikiwamo kukemea vitendo viovu vinavyohatarisha usalama, amani na misingi ya Taifa.

Akizungumzia amani ya nchi, Sumaye aliwataka Watanzania kukemea vitendo viovu vinavyolikumba taifa bila kujali kama kukemea huko kutawaudhi wenye mamlaka na nguvu za fedha.

Alisema taifa litaangamia iwapo hali ya uhasama wa kiimani, kiitikadi na maeneo mabomu kutupwa kwenye mikusanyiko ya watu kwa nia ya kuua, itaachwa iendelee.

“Taifa linakabiliwa na matatizo mengi. Watu wamefikia hatua ya kuchukiana kwa sababu ya imani zao. Mabomu yanalipuliwa katika mikusanyiko ya jamii na kuteketeza watu wasio na hatia,” alisema Sumaye na kuongeza:

“Je, tumekuwa na ujasiri wa kukemea mabaya hata kama kukemea huko kunawaudhi au kuwakera wenye mamlaka au na wenye nguvu za fedha?”

Sumaye alihoji kilichotokea hadi leo Watanzania waanze kubaguana kwa maeneo wanakotoka, viongozi wa dini kuuawa, makanisa kuchomwa moto na Wakristo na Waislamu kupigana kugombea nani achinje mnyama.

“Haya yote ni mambo mageni nchini mwetu, tuendelee kuiombea nchi yetu amani lakini wakati maombi yakiendelea, Watanzania tujue tunajichimbia kaburi letu wenyewe kama hatutapiga vita maovu haya,” alisema.

Sumaye aliyekuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 ya Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, alihoji uadilifu na dhamira ya Watanzania, wakiwamo viongozi wa dini ambao hivi sasa wanawasifia na kuwakumbatia watu wanaotoa michango mikubwa ya fedha madhabahuni bila kujali uadilifu wao na jinsi walivyochuma fedha hizo.

Mkuu wa KKKT, Askofu Alex Malasusa alisema Kanisa halitaogopa kusema ukweli pale panapobidi huku akiahidi kuwa litaendelea kujenga marafiki wema bila kujali itikadi zao kisiasa wala ukwasi.

Sherehe hizo zilihudhuriwa pia na viongozi wa Kiislamu kitendo ambacho Askofu Malasusa alisema ni ishara ya ushirikiano na uhusiano mwema kati ya dini na madhehebu yote nchini tofauti na chuki inayojaribu kupandikizwa na wasiolitakiwa mema taifa.

CHANZO: www.mwananchi.co.tz